IQNA

Hija 1445

Hija: Zaidi ya Waislamu milioni 1.2 wawasili Saudi Arabia, joto laongezeka

9:41 - June 08, 2024
Habari ID: 3478947
IQNA - Zaidi ya Waislamu milioni 1.2 tayari wamewasili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya Hija ya kila mwaka huku hali ya joto ikiongezeka.

Mwaka huu, zaidi ya Waislamu milioni 2 kutoka kote ulimwenguni wanatarajiwa kushiriki katika ibada ya Hija, ambayo kulingana na muandamo wa mwezi wa Saudi itaanza Juni 14.

Ofisi ya Miradi ya Hija inashirikiana na mashirika zaidi ya 50 ya serikali kutekeleza mipango 300 katika maeneo 2,600. Waziri wa Hijja na Umra wa Saudia, Tawfiq Al Rabiah, alisema tangu kumalizika kwa Hija ya mwaka jana, timu yake imetembelea nchi 11 kujadili uwekezaji katika miradi inayolenga kusaidia mahujaji na kutatua changamoto zinazowezekana.

Mpango mmoja kama huo ni Njia ya Makka, inayotumiwa na mahujaji 250,000. Njia hii inaruhusu wasafiri kutoka viwanja vya ndege 11 katika nchi saba - Pakistan, Malaysia, Indonesia, Morocco, Bangladesh, Uturuki, na Ivory Coast - kukamilisha taratibu za kuingia Saudi Arabia katika viwanja vyao vya nyumbani, na hivyo kuwapa idhini ya kwenda moja kwa moja Makka na. Madina.

Hata hivyo, Hija ya mwaka huu inatoa changamoto ya kipekee - joto kali.

Huku halijoto ikitarajiwa kuzidi 44ºC, mkuu wa kituo cha kitaifa cha hali ya hewa Saudia Ayman Ghulam alionya juu ya ongezeko la wastani la joto la nyuzi joto moja na nusu hadi mbili juu ya kawaida huko Makka na Madina. Pia alitabiri unyevu wa kiasi wa asilimia 25, viwango vya mvua karibu na sufuri, na wastani wa kiwango cha juu cha joto cha 44ºC.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Abdulrahman Al Sudais, Mkuu wa Urais wa Masuala ya Dini kwa Msikiti Mkuu na Msikiti wa Mtume (Al Masjid An Nabawi), amewataka wahubiri na maimamu kufupisha hotuba zao na sala ya Ijumaa ya adhuhuri.

Ili kupunguza zaidi athari za joto, mamlaka ya Saudia imetekeleza hatua kama vile kunyunyiza maji barabarani na njia za watembea kwa miguu, na kuweka feni na miavuli yenye kunyunyiza maji katika mahali patakatifu. Mahujaji pia wanashauriwa kuwa na maji ya kunywa wakati wote na kuchukua tahadhari dhidi ya hali ya hewa ya joto.

Wakati huo huo wakuu wa Saudia wakibaini kuwa  takriban Waislamu milioni 30, wa ndani na wa kimataifa, walishiriki katika ibada ya Umra au Hija ndogo katika Msikiti Mkuu wa Makka katika mwezi mtukufu wa Kiislamu uliopita wa Ramadhani.

3488650

Habari zinazohusiana
Kishikizo: hija
captcha