IQNA

Hija

Msomi wa Kanada: Hija ni mkusanyiko mkubwa zaidi wa amani, mshikamano na Palestina

18:57 - June 11, 2024
Habari ID: 3478962
IQNA - Mwanafikra na Mtaalamu wa Uislamu kutoka Kanada ameitaja Hija kama sio tu ibada lakini mkusanyiko mkubwa zaidi wa amani duniani.

Akihutubia Kikao cha intaneti (webinari) chini ya anuani ya "Hija; Mhimili wa Qur'ani na Kufungamana na Gaza",  John Andrew Morrow alisema fursa ya Hija inapaswa kutumika kuonesha nguvu ya Umma wa Kiislamu na sauti ya mshikamano na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Semina hiyo ya mtandaoni iliandaliwa na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) Jumatatu Juni 10.
Andrew Morrow, ambaye amechagua jina la Ilyas Abdul Alim Islam baada ya kuwa Muislamu, alisema Hija inaakisi imani ya Mungu mmoja pamoja na umoja wa kibinadamu, kidini na kijamii.
Ameongeza kuwa, Waislamu wanapaswa kuzingatia nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa za Hija na vilevile mielekeo yake ya kidini.
Wanapaswa kukumbatia na kufanyia kazi kanuni za kimaadili na kitabia zinazofundishwa na Qur'an na Mtukufu Mtume (SAW), alisema.
Msomi huyo wa Kanada alisema Hija pia ni fursa bora ya kujifunza, kuendeleza urafiki na kujenga uhusiano wa kirafiki.
Kwingineko katika maelezo yake, alisema watu wote wenye mantiki, wawe Waislamu, Mayahudi, Wakristo, n.k, wanaunga mkono Palestina na kulaani uhalifu wa kivita wa Israel na ukiukaji wa haki za binadamu.
Akisisitiza umuhimu wa kupinga jinai na mauaji ya kimbari, alinukuu Aya ya 32 ya Sura Al-Maidah ya Qur’ani Tukufu isemayo, “Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi."
Andrew Morrow pia alisema Uislamu wa kweli ni Uislamu wa kustahamiliana na wa wastani, kama Quran Tukufu inavyosema, “Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu.” (Aya ya 143 ya Surah Al -Baqarah)
Profesa wa Chuo Kikuu cha Tehran Mohammad Ali Azarshab, Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini Lebanon Sheikh Ghazi Hunaina, Mkuu wa Umoja wa Wanazuoni wa Ahl al-Bayt wa Uturuki Ghadir Akaras, na Mkuu wa Baraza la Ushauri la Jumuiya za Kiislamu la Malaysia (MAPIM) Muhammad Azmi Abdulhamid walikuwa miongoni mwa wazungumzaji wengine kwenye webinari hiyo.

3488699

Kishikizo: hija iqna
captcha