IQNA

Arbaeen

Mbunge Marekani atakiwa kukutana na Waislamu baada ya malumbano ya video ya Arbaeen

22:19 - August 30, 2024
Habari ID: 3479351
IQNA - Mwakilishi wa Jimbo la Utah nchini Marekani Trevor Lee amehimizwa kukutana na Waislamu wa jimbo hilo baada ya video aliyochapisha kusababisha wimbi la chuki dhidi ya Uislamu.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), Jumatano lilimtaka mbunge wa jimbo hilo kukutana na Waislamu na kujenga maelewano zaidi.

Katika mtandao wa kijamii wa X, Mwakilishi Lee alichapisha video ya kundi la Waislamu wa madhehebu ya  Shia huko Taylorsville katika matembezi ya Arbaeen, ambayo inaadhimisha siku ya 40 baada ya Ashura, kumbukumbu ya kuuawa shahidi wa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS).

Lee aliandika katika mtandao wa X kwamba  "hakuna bendera moja ya Amerika inayoonekana." Chapisho hilo lilikutana na majibu mengi dhidi ya Uislamu.

"Sikuwa nikijaribu kuwasilisha chochote isipokuwa hiyo ni video ya kupendeza," Lee alisema kwenye mahojiano. "Huu ni mji mdogo wa Taylorsville, Utah, na sijawahi kuona matembezi kama haya maishani mwangu hapo awali." "Pande zote zina dhana mbaya, iwe ni marengo ya kulia au kushoto," Lee alisema na kuongeza kuwa hakuwa na nia mbaya katika kusambaza video hiyo.

Kituo cha Kiislamu cha Alrasool kilisema kuwa Mwakilishi Lee na wabunge wengine wanakaribishwa kutembelea na kukutana na wanajamii ili kupata ufahamu bora wa Uislamu hasa madhehebu ya Shia.

“Ni muhimu kwa viongozi waliochaguliwa kujua na kuelewa makundi yote ya maeneobunge yao. Tunamtia moyo Mwakilishi Lee kuafiki pendekezo la mkutano na jumuiya ya Waislamu ili kujenga uelewa zaidi,” alisema Mkurugenzi wa Utafiti na Utetezi wa CAIR Corey Saylor.

Alibainisha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2024, CAIR ilisajili malalamiko 4,951 ya chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia, ongezeko la asilimia sitini na tisa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

3489695

captcha