IQNA

Waislamu Wamarekani waishtaki FBI kwa orodha ya 'siri' ya kutotumia ndege

16:13 - September 19, 2023
Habari ID: 3477622
TEHRAN (IQNA)- Kundi la utetezi wa Waislamu nchini Marekani limeishtaki Idara ya Upelelezi, FBI, katika jaribio la kukomesha utumizi wa orodha ya siri ambayo aghalabu inalenga Waislamu pekee kwa uchunguzi wanaposafiri kwa ndege.

Kesi hiyo imewasilishwa na Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR), dhidi ya mashirika 29 ya Marekani, ikiwa ni pamoja na Idara ya Sheria, FBI, Kikosi cha Ulinzi cha Siri, Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka, na Idara ya Usalama wa Uchukuzi.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika makao makuu ya CAIR mjini Washington, D.C., wakili Hannah Mullen alidai kuwa orodha hiyo inatumika kuwalenga na kuwabagua Waislamu.

Mullen alisema, "Serikali ya shirikisho inachukulia ukweli wa kuwa Muislamu kuwa wa kutiliwa shaka na inawaweka watu kwenye orodha ya waangalizi kutokana na utambulisho wao wa Kiislamu, imani ya dini ya Kiislamu, desturi za dini ya Kiislamu, kusafiri katika nchi nyingi za Kiislamu, na mambo mengine ya kibaguzi."

Aliongeza kuwa, hakuna mteja wetu ambaye amewahi kufunguliwa mashtaka au kuhukumiwa kwa uhalifu unaohusiana na ugaidi."

Orodha hiyo iitwayo ya ugaidi, ambayo iliwekwa mtandaoni na mdukuzi wa Uswizi mwezi Januari, inajumuisha zaidi ya majina ya watu milioni 1.5 ambao serikali inawaita "magaidi wanaojulikana au wanaoshukiwa."

Orodha hiyo iliyotangazwa mwaka wa 2019 ilionyesha kuwa FBI imekuwa ikilenga isivyo sawa jamii ya Waislamu kwani ilikuwa na majina mengi ya Kiislamu na Kiarabu.

Dina Sayed-Ahmed, meneja wa mawasiliano katika kitengo cha New Jersey ya CAIR, alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Newark, New Jersey, Jumatatu kwamba Waislamu nchini Marekani wanachukuliwa kama "raia wa daraja la pili."

"Matokeo [ya orodha kama hiyo] ni kwamba watu wasio na hatia wanaweza kukaa kwenye orodha ya washukiwa kwa muda usiojulikana.

 Meya wa chama cha Democratic kutoka New Jersey Mohamed Khairullah ambaye ni Muislamu na alizuiwa kuingia Ikulu wa White House mapema mwaka huu anapanga kuishtaki serikali ya Marekani.

Hivi sasa analenga kukomesha orodha ya ugaidi ya serikali ya shirikisho ambayo hapo awali alisema inalenga Waislamu  bila haki- ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe katika majira ya joto wakati alipozuiwa kuingia katika Ikulu ya White House.

Khairullah amesema "usumbufu na unyanyasaji huo si jambo la kawaida" kwake. Mnamo mwaka wa 2019, Khairullah alisema alizuiliwa kwa saa nyingi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK huko New York na kuulizwa ikiwa anajua magaidi wowote na akalazimika kupeana simu yake ikaguliwe. Lakini alisema amekuwa Ikulu ya White House hapo awali bila shida.

3485228

Habari zinazohusiana
Kishikizo: marekani cair
captcha