Katika taarifa, Hamas iliwaalika Waislamu kuswali katika misikiti na vituo vya Kiislamu kote ulimwenguni kwa ajili ya Sinwar kama kumbukumbu kwa kiongozi mkuu wa kitaifa na Kiislamu wa Palestina ambaye aliuawa shahidi katika njia ya kulinda ardhi takatifu ya Palestina na Msikiti wa Al-Aqsa.
Aidha imetoa wito wa kufanyika maandamano ya hasira dhidi ya utawala wa Israel.
Wakati huo huo, Harakati ya Jihadi Islami ya kupigania ukombozi wa Palestina nayo imelaani kitendo cha utawala haramu wa Israel cha kumua Sinwar.
Jihad Islami imeyataka makundi na mirengo yote ya Palestina kusimama kidete kukabiliana na utawala wa Kizayuni ambao umeanzisha vita vya mauaji ya halaiki huko Palestina na unatekeleza jinai dhidi ya binadamu.
Harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya Palestina (Fat'h) pia ilisema katika kujibu mauaji ya Shahidi Sinwar kwamba kwa kutumia ugaidi na mauaji, Israel haiwezi kufuta matakwa ya watu wa Palestina ya kurejesha haki zao halali na kupatikana kwa uhuru na uhuru.
Sinwar alipatikana amekufa shahidi katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza siku ya Alhamisi, akiwa amevalia fulana ya kivita na bunduki aina ya AK-47 kando yake.
Sinwar alitumia umri wake wote wa miaka 62 kuendesha mapambano dhidi ya utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu. Sinwar alifungwa miaka 23 katika jela za utawala wa Kizayuni. Utawala wa Kizayuni ulibomoa nyumba yake katika vita vya mwaka 2012, na mnamo mwaka 2015 pia Yahya Sinwar akawekwa katika orodha nyeusi ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani. Sinwar kwa muda mrefu aliwekwa katika orodha ya watu wanaosakwa na Israel; na ari ya Israel ya kutaka kumuua iliongeza hivi karibuni baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas. Vyombo vya usalama vya Israel vinaamini kuwa Sinwar alihusika katika kuratibu na kutekeleza mashambulio ya Oktoba 7 mwaka jana. Baada ya oparesheni ya "Kimbunga cha al Aqsa", jina la Sinwar lilitajwa mara kwa mara na maafisa waandamizi wa utawala wa Israel akiwemo Waziri wa vita wa utawala huo Yoav Galant.
Utawala wa Kizayuni ulijaribu kumvunjia heshima Sinwar kwa kumzulia uwongo chungu nzima kama vile eti alikuwa amejificha kwenye mahandaki na kuwatoa mhanga wakazi wa Gaza, na kwamba alikuwa amewateka nyara raia wa utawala wa Kizayuni au kwamba alikuwa amekimbilia nchini Misri. Kosa la kistratejia la Wazayuni la kurusha picha na video zinazooyesha namna Sinwar alivyouliwa shahidi limeibua kashfa kwa Wazayuni na kupelekea jina la Sinwar kusalia hai katika historia.
Picha za kuuawa shahidi Yahya Sinwar, kiongozi wa harakati ya Hamas, ambaye alikuwa katika medani ya vita akiwa amevalia sare za mapambano na kukabiliana na utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho ya maisha yake, zimeonyesha kuwa alikuwa shujaa wa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni.
3490342