Shahidi Haniya aliuawa kigaidi na utawala wa Kizayuni hapa mjini Tehran tarehe 31 Julai, siku moja baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.
Kuchaguliwa Yahya Sinwar, mwenye umri wa miaka 61, kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kumeibua mshangao, hofu na wahaka mkubwa kwa utawala wa Kizayuni.
Yahya Ebrahim Sinwar,alyezaliwa katika kambi ya wakimbizi ya Gaza, kusini mwa Khan Younis, ndiye mwanzilishi wa idara ya usalama ya Hamas, iliyopewa jina la "Majd", inayoshughulikia kesi za usalama wa ndani. Utawala wa Kizayuni ulifeli katika shambulio la kigaidi la kutaka kumuua Sinwar.
Miaka ya Harakati
Sinwar alijiunga na Harakati ya Ikhwanul Muslimin (Muslim Brotherhood) akiwa na umri mdogo na alisoma katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza, ambako alipata shahada ya kwanza ya Kiarabu. Katika miaka yake ya chuo kikuu, aliongoza "Mrengo wa Kiislamu," mrengo wa wanafunzi wanachama wa Ikwanul Muslimin.
Mnamo 1982, jeshi katili la Israeli lilimkamata Sinwar kwa mara ya kwanza na kumwachilia baada ya siku chache, na kumkamata tena baadaye mwaka huo, na kumhukumu kifungo cha miezi sita jela kwa "kushiriki katika shughuli dhidi ya Israeli."
Mnamo Januari 20, 1988, Israel ilimkamata tena na kumhukumu vifungo vinne vya maisha pamoja na miaka 30 kwa "kuanzisha chombo cha usalama cha Al-Majd na kushiriki katika uanzishaji wa tawi la kwanza la kijeshi la Hamas, lililojulikana kama Mujahidina wa Palestina."
Miaka 23 Jela
Sinwar alikaa miaka 23 katika magereza ya kuogofya ya utawala haramu wa Israel kabla ya kuachiliwa kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Hamas na Israel mwaka 2011 katika mapatano yaliyopewa jina la 'Mapatano ya Shalit." Chini ya makubaliano yaliyotekelezwa tarehe 11 Oktoba 2011 kati ya Hamas na utawala haramu wa Israel, utawala huo uliwaachilia wafungwa 1,027 wa Kipalestina ili kubadilishana na kuachiliwa kwa mwanajeshi Muisraeli Gilad Shalit.
Kabla ya kuachiliwa kwake Sinwar aliweza kuwakusanya na kuwaunganisha wafungwa wa Kipalestina na kufanya mikutano ya siri kati yao bila kuweza kutambuliwa na vyombo vya usalama vya Israel. Pia inasemekana kwamba alijifunza Kiebrania alipokuwa gerezani, kulingana na maelezo ya mfungwa wa zamani wa Fat'h ambaye alitumikia muda na Sinwar.
Baada ya kuachiliwa kwake mwaka 2011, Sinwar alishiriki katika uchaguzi wa ndani wa Hamas mwaka 2012, akishinda kiti katika ofisi ya kisiasa na kuchukua jukumu la kusimamia tawi la kijeshi la kundi hilo, Brigedi za Izzudin Al-Qassam.
Marekani yamlenga
Mnamo Septemba 2015, Marekani ilimuweka Sinwar kwenye orodha yake ya "magaidi wa kimataifa." Idara za usalama za Israeli pia zimeorodhesha Sinwar kama mmoja wanaopaswa kuuawa huko Gaza.
Alichukua nafasi muhimu katika kuandaa Maandamano Makuu ya Kurejea na Kuvunja Maandamano ya Kuzingirwa huko Gaza mwaka 2018, ambayo yalivuta hisia za kimataifa kwenye mapambano ya Wapalestina na kuona wito wa kimataifa wa kuishinikiza Israel kuondoa vikwazo vyake dhidi ya Gaza.
Uteuzi wenye kuimarisha Muqawama
Kuchaguliwa Yahya Sinwar kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa ya Hamas kumepokewa kwa hisia mbalimbali katika eneo na dunia, na baadhi wameuchukulia uteuzi huu kuwa ni wa kuimarisha muqawama na kuendeleza njia ya shahidi Ismail Haniyeh.
Shirika la Utangazaji la Israel limesema kuwa, uteuzi wa Sinwar unashangaza na ni ujumbe kwa Israel kwamba yu hai na kwamba uongozi wa Hamas huko Gaza uko imara, upo na utabakia.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati wa gazeti la Times of Israel, Avi Iskharov, amesema kuwa harakati ya Hamas imechagua "mtu hatari zaidi kuiongoza," hasa kwa vile Israel inamtambua Sinwar kuwa mhandisi wa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa Oktoba 7 mwaka jana (2023), ambayo ilitoa kipigo kikubwa kwa jeshi la utawala huo, na kuchafua taswira ya idara zake za kijasusi na kiusalama mbele ya macho ya walimwengu.
Nayo televisheni rasmi ya Israel, Kan, imesema kuwa uteuzi wa Sinwar kushika nafasi ya Ismail Haniya unaonyesha kuwa Hamas bado ina nguvu na ni imara huko Gaza.
Osama Hamdan, mmoja wa wanachama waandamizi wa Hamas amesema kuhusiana na suala hili kwamba: Kuchaguliwa haraka Sinwar kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa kwa kauli moja kunaonyesha nguvu na uimara wa Hamas.
Hamdan amesisitiza kuwa: "Ujumbe wa Hamas ni kwamba imemchagua kuwa kiongozi wake mtu ambaye amekuwa mtunza amana katika jihadi na mapambano katika medani ya vita huko Gaza kwa zaidi ya siku 300."
Yahya Sinwar amechaguliwa kuwa mkuu mpya wa ofisi ya kisiasa ya Hamas katika hali ambayo bado anaishi Gaza licha ya hujuma na vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda huo.
Hatua ya Hamas ya kumteua Sinwar inaonesha kuwa, makundi ya muqawama ya Palestina bado yanaona kuwa, muqawama na kusimama kidete dhidi ya Wazayuni ndio chaguo lao kuu la kufikia malengo ya kistratijia na kisiasa.
Mkuu huyo mpya wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ana historia ndefu ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni, na pia anatajwa kuwa mbunifu na kiongozi wa operesheni ya "Kimbunga cha Al-Aqswa ".
Mwenendo wa matukio ya vita vya Gaza umeleta uthabiti na mshikamano zaidi kati ya makundi ya wapiganaji wa Palestina. Katika hali hiyo, kuchaguliwa Yahya Sinwar kutapelekea mshikamano na ushirikiano zaidi wa makundi ya muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni.
423060