IQNA

Wafuasi milioni moja wa Imam Mahdi (AS) wajumuika katika usiku wa Katikati ya Shaaban

16:16 - February 13, 2025
Habari ID: 3480212
IQNA – Mkusanyiko wa wafuasi na maashiki wa Imam Mahdi (AS) unaendelea katika Msikiti wa Jamkaran, Qom, Iran, usiku wa Iddi ya Katikati ya Shaaban maarufu kama Nisf Shaaban.

Sherehe hii inayotarajiwa kuvutia umati wa watu milioni moja unafanyika Alhamisi jioni, kuanzia saa kumi na mbili jioni, katika Uwanja wa Imam Mahdi (AS) ndani ya Msikiti huo.

Mjumuiko huo ujumuisha mipango mbalimbali ikiwemo usomaji Qur'ani Tukufu,  mashairi, qaswida.

Baada ya Sala za  Maghrib na Isha, mhubiri mkuu Hujjatul Islam Masoud Aali atatoa hotuba, kisha kutakuwa na usomaji wa mashairi.

Maadhimisho hayo yatakamilishwa na milipuko ya fataki usiku wa manane kama ishara ya sherehe ya kuzaliwa kwa Imam Mahdi (AS) katika Msikiti wa Jamkaran.

Ijumaa mwezi 15 Shaaban 1446  Hijria sawa na tarehe 13 Februari 2025 inasadifiana na kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Imam wa Zama hizi, Imam Mahdi (AS) na Imam wa 12 wa Waislamu wa Kishia.

Siku kama hii  miaka 1191 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (AS) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra, kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq.

Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (AS) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (SAW). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa, na al Qaim, kwa maana ya atakayeanzisha mapambano.

Imam Mahdi (AS) alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa chini ya malezi ya baba yake mpendwa, Imam Askari (AS). Alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu na kisha akatoweka na kwenda ghaiba kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu.

Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi (AS) alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu na atadhihiri tena ulimwenguni wakati mwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa.

Atakapodhihiri duniani, ataijaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huadhimishwa nchini Iran kama Siku ya Waliodhulumiwa Duniani. 

Tunatoa mkono wa kheri na baraka kwa wapenda haki wote na hasa wafuasi wa kweli wa Ahlul Bayti wa Bwana Mtume Muhammad (SAW) kwa mnasaba wa kuchomoza nuru hiyo ya haki.

349184

captcha