IQNA

Mwokozi katika Qur’ani Tukufu / 1

Aya ya Qur’ani Inayohusu Jamii ya Imam Mahadi au Mahdawiyya

11:54 - February 05, 2026
Habari ID: 3481892
IQNA – Aya ya 55 ya Surat An-Nur inaeleza juu ya jamii tukufu ambayo bado haijawahi kutimia kikamilifu katika ulimwengu huu, wala haiwezi kutekelezwa juu ya jamii yoyote ile isipokuwa ile itakayoundwa kwa baraka ya kudhihiri kwa Imamu Mahdi (AS).

Qur’ani Tukufu yasema katika Aya ya 55 ya Surat An-Nūr:

“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.”

Aya hii imewaelekea Waislamu wote kwa ujumla, ambao miongoni mwao wapo wanafiki na waumini; na miongoni mwa waumini wapo wanaotenda mema na wasiokuwa hivyo. Ahadi iliyotajwa katika aya hii inawahusu kikhsusi kundi la pili—yaani wale walioamini kwa dhati na wakatenda mema.

Maana ya “Ukhalifa” (uongozi au uwakala) katika aya hii ni kuwakabidhi ardhi na kuwafanya watawale na kutawala juu yake, kama Mwenyezi Mungu Alivyosema kwa maana hii:

“Ardhi ni ya Mwenyezi Mungu; humrithisha amtakaye katika waja Wake.” (Surat Al-A‘rāf, Aya 128)

Na pia Amesema:

“Na bila shaka waja Wangu wema watairithi ardhi.” (Surat Al-Anbiyā’, Aya 105)

Kwa mujibu wa ufahamu huu, maana ya “makhalifa waliokuwa kabla yao” ni waumini wa mataifa yaliyotangulia, kama kaumu za Nabii Nuh (AS), Hud (AS), Ṣaliḥ (AS) na Shu‘ayb (AS).

Kwa muhtasari, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaahidi wale walioamini na wakatenda mema kwamba Atawajaalia kwa haraka jamii iliyo njema kwa kila upande, jamii iliyo huru kabisa na uchafu wa ukafiri, unafiki na maovu; jamii itakayoirithi ardhi, na katika itikadi na matendo ya watu wake haitatawala chochote isipokuwa dini ya haki.

Wataishi katika amani na usalama, bila ya khofu ya adui wa ndani wala wa nje; wataepushwa na hila za wadanganyifu, dhulma za madhalimu na jeuri za madikteta.

Jamii kama hiyo ya fadhila haijawahi kutimia katika historia ya ulimwengu, wala dunia haijashuhudia mfano wake tangu siku aliyotumwa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kama Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Basi iwapo kuna mfano wake, hautakuwa ila katika zama za Mahdi Aliyeahidiwa (Mwenyezi Mungu Aharakishe kudhihiri kwake), kwa sababu Hadithi Mutawatir kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kuhusu sifa za Imamu huyo zinatoa habari ya kutimia kwa jamii ya namna hiyo.

Huenda baadhi wakauliza: kwa nini aya hii iliwaelekea wakati wa kushuka kwake kwa kauli “wale miongoni mwenu walioamini na wakatenda mema” ilhali Imamu Mahdi (AS) hakuwepo katika zama hizo?

Habari ya Inayohusiana:

Swali hili linatokana na kuchanganywa kwa anwani za mtu mmoja mmoja na anwani za kijamii. Anwani zipo aina mbili: ya kwanza ni kumwelekea mtu binafsi kwa kuzingatia sifa zake binafsi; ya pili ni kumwelekea watu wale wale, lakini kwa kuzingatia kuwa wao ni kundi lenye sifa maalumu. Katika aina ya pili, watu binafsi hawakusudiwi kwa nafsi zao, bali hukusudiwa yeyote mwenye sifa hizo. Anwani nyingi za Qur’ani kwa waumini au makafiri ni za aina hii.

Kwa mfano, ahadi iliyotolewa kwa Mayahudi:

“Basi itakapokuja ahadi ya uharibifu wenu wa pili, nyuso zenu zitatiwa huzuni.” (Surat Al-Isra’, Aya 7)

Au kauli ya Dhul-Qarnayn:

“…itakapokuja ahadi ya Mola wangu Ataifanya tambarare; na ahadi ya Mola wangu ni kweli daima.” (Surat Al-Kahf, Aya 98)

Hivyo basi, tukitaka kubainisha maana halisi ya Aya ya 55 ya Surat An-Nūr, na kuacha kando mapendeleo na upendeleo wa kimtazamo, aya hii tukufu haiwezi kutekelezwa juu ya jamii yoyote ile isipokuwa jamii ambayo itatimia hivi karibuni kwa baraka ya kudhihiri kwa Imamu Mahdi (AS).

3496298

captcha