IQNA

Kiongozi wa Hizbullah atajwa kuwa “Msaidizi wa Imam Mahdi" wa mwaka

20:42 - February 04, 2026
Habari ID: 3481891
IQNA – Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametangazwa rasmi kuwa “Mahdi Yavar" yaani Msaidizi wa Imam Mahdi' wa Mwaka.

Tangazo hilo lilitolewa katika mkesha wa Sikukuu ya Nisf Sha’ban, inayoadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Imam Zaman (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).

Sheikh Qassem alichaguliwa kuwa Mahdi Yavar wa Mwaka na Msikiti mtukufu wa Jamkaran wa Qum, Iran kutokana na shughuli zake bora na mchango wake mkubwa katika kuendeleza mjadala wa Mahdawi (itikadi ya Imam Mahdi), pamoja na kusimama imara katika njia ya mapambano na Muqawama..

Uteuzi huo ulifanywa kwa kutambua juhudi zake endelevu katika kuwatetea waliodhulumiwa, kukabiliana na mikondo ya kiburi na ubeberu, na kuimarisha safu ya haki.

Sherehe ya kumtambulisha Mahdi Yavar wa Mwaka inayoratibiwa na Msikiti wa Jamkaran hufanyika kwa lengo la kuwaenzi watu wanaochangia kikamilifu katika kufufua mjadala wa Mahdawi na kuimarisha utamaduni wa kumsubiri Mwokozi Aliyeahidiwa.

Katika hafla hiyo, mchango wa watu wenye ushawishi katika kukuza utamaduni wa kungojea Mwokozi hutambuliwa na kuthaminiwa.

Katika miaka ya karibuni, watu kadhaa mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu wamechaguliwa kuwa Mahdi Yavar, wakiwemo Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, Sheikh Ibrahim Zakzaky, Jenerali Hajj Qassem Soleimani, Abu Mahdi al-Muhandis, Ayatollah Sheikh Isa Qassim, Jenerali Mstaafu Ali Fazli, pamoja na Hujjat al-Islam Hashem al-Haydari.

Sikukuu ya Kati ya Sha’ban, inayoadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Imam Zaman (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), huangukia siku ya 15 ya mwezi wa Sha’ban katika kalenda ya Hijria.

Waislamu wa madhehebu ya Shia kote ulimwenguni waliadhimisha tukio hilo tukufu siku ya Jumatano, tarehe 4 Februari, mwaka huu.

Habari inayohusiana:

Siku kama ya leo miaka 1192 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (AS) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra, kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari AS ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (SAW). 

Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa, na al Qaim, kwa maana ya atakayeanzisha mapambano.Imam Mahdi AS alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa chini ya malezi ya baba yake mpendwa, Imam Askari AS.

Alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu na kisha akatoweka na kwenda ghaiba kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu.

Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi (AS) alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu na atadhihiri tena ulimwenguni wakati mwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa.

Atakapodhihiri duniani, ataijaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huadhimishwa nchini Iran kama Siku ya Waliodhulumiwa Duniani. 

4332346

Habari zinazohusiana
captcha