IQNA

Waumini waanza kuwasili Saudia kwa ajili ya Hija huku kukiwa na picha nadra za Kaaba

17:19 - May 02, 2025
Habari ID: 3480626
IQNA – Waumini wanaokusudia kutekeleza Ibada ya Hija wanaendelea kuwasili Saudi Arabi na kupokelewa katika Msikiti Mkuu wa Makka, ambapo makundi ya awali yaliwasili mnamo Aprili 30.

Kama sehemu ya mapokezi hayo ya waumini hao yaliyoandaliwa na Idara ya Masuala ya Kidini Makka, wageni wa Mwenyezi Mungu walipokea zawadi na vifaa vya kielimu kwa lugha mbalimbali vinavyohamasisha mitazamo ya wastani, amani, na umoja miongoni mwa Waislamu.
Wakati huohuo, video nadra zimeibuka zikionyesha eneo la mataf — sehemu inayozunguka Kaaba — likiwa karibu tupu, jambo adimu kabla ya msimu wa Hija kuanza.
Ni idadi ndogo tu ya waumini wa kigeni, waliofika siku ya kwanza ya ruhusa ya kuingia, walionekana wakitekeleza ibada ya tawaf, yaani kuizunguka Kaaba kama desturi ya ibada.

Uwepo mdogo wa waumini unatokana na masharti makali ya kuingia yaliyowekwa na mamlaka za Saudi Arabia kujiandaa kwa Hija ya mwaka 1446H (2025). Tangu Aprili 29, ni wale tu wenye visa za Hija au vibali rasmi waliokuwa wakiruhusiwa kubaki au kuingia Makka.
Wizara ya Utalii imezielekeza kampuni za usafiri na huduma za malazi katika mji mtakatifu kutochukua au kuhifadhi wageni wasio na nyaraka halali za Hija, vibali vya kazi, au ukaazi.

Hatua hizi zinafuatia agizo la awali la Usalama wa Umma lililowazuia wahamiaji wasio na vibali kuingia Makka kuanzia Aprili 23.
Masharti haya ni sehemu ya juhudi pana kuhakikisha usalama, ulinzi, na ufanisi wa harakati za Mahujaji. Mamlaka pia zimethibitisha kwamba Aprili 29 ilikuwa siku ya mwisho kwa mahujaji wa Umra kuondoka nchini, na sasa wote wasio na visa za Hija wamezuiwa kubaki Makka.

Aidha, vibali vya Umra kupitia jukwaa la Nusuk vimesitishwa hadi Juni 10 kwa wote, wakiwemo raia wa Saudi Arabia, wakaazi, na wenye visa nyingine. Kadri msimu wa Hija unavyoendelea, idadi ya mahujaji katika Msikiti Mkuu inatarajiwa kuongezeka katika siku zijazo huku waumini zaidi kutoka duniani kote wakiwasili.

 

3492903

Kishikizo: saudi arabia makka hija
captcha