Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari Jumanne, Alireza Bayat Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara la Iran amesema maandalizi yamekamilika kwa safari ya wananchi wa Iran kuelekea maeneo matakatifu Saudi Arabia. "Operesheni ya kuwasafirisha waumini kuelekea Hija itaanza Mei 5 na itaendelea hadi Mei 31," amebaini.
Kwa mujibu wa Bayat, takriban wasafiri 4,000 wa Hija wataondoka kila siku kutoka Iran, huku safari za kurudi zikitarajiwa kukamilika ndani ya siku 20. Mashirika ya ndege ya Iran Air na Flynas ya Saudi Arabia yatashiriki katika kusafirisha wanaoelekea Hija. Mwaka huu, vikundi 575 vya mahujaji vimeundwa, ambapo asilimia 58 wataanza na Madina na asilimia 42 wataanza na Makka.
Bayat ametoa maelezo ya kidemografia, akibainisha kuwa asilimia 54 ya Wairani wanaoelekea Hija ni wanawake na asilimia 46 ni wanaume. "Takriban asilimia 51 miongoni mwao wako chini ya umri wa miaka 55," amesema.
Kuhusu mipango ya suhula za Mahujaji Wairani nchini Saudia, Bayat amesema kuna maeneo makuu manne ya kutayarisha chakula ambao mawili yako Makka na mawili mengine yako Madina. Inatazamiwa kuwa maeneo hayo yatatayrisha zaidi ya milo milioni saba kwa ajili ya Mahujaji Wairani.
Aidha amegusia pia suala la Mahujaji wanaorejea nyumbani kubeba maji ya Zamzam na kusema: "Mwaka huu, kila aliyetekeleza ibada ya Hija atapokea lita tano za maji ya Zamzam ambayo atakabidhiwa baada ya kurudi Iran.”
Mipango ya malazi inajumuisha hoteli 19 Madina, zote zikiwa karibu na Al Masjid An Nabawi au Msikiti wa Mtume, na hoteli 57 Makka. "Kwa kuzingatia umbali kutoka baadhi ya hoteli hadi Masjid al Haram, huduma ya basi la safari saa 24 itapatikana," ameongeza.
Bayat amebainisha kuwa katika eneo la Mina kutakuwa na nafasi ndogo na hivyo amesema: "Tunaomba Mahujaji wawe na uangalifu kwa wenzao. Kwa sababu joto linatarajiwa kuzidi nyuzi joto 52°C, tumeingia mkataba na kampuni ya Saudi kwa ajili ya kuweka viyoyozi ili kuboresha faraja wakati wa kukaa eneo hilo," amesema.
Takriban Wairani 85,000 watashiriki katika ibada za Hija mwaka huu.
Hija ni ibada ya kwenda Makka ambayo kila Mwislamu mwenye uwezo wa kimwili na kifedha analazimika kuitekeleza angalau mara moja katika maisha yake.