IQNA

Hija 1446: Zaidi ya Waislamu milioni moja wawasili Saudia

17:34 - May 27, 2025
Habari ID: 3480749
IQNA – Zaidi ya Waislamu milioni moja kutoka nje ya Saudi Arabia wamewasili katika ufalme huo kwa ajili ya kushiriki katika ibada ya Hija ya kila mwaka, mamlaka husika zimetangaza siku ya Jumatatu.

Hija 1446: Zaidi ya Waislamu milioni moja wa kimataifa wawasili SaudiaWaziri wa Habari wa Saudi Arabia, Salman bin Yousef al-Dosari, alithibitisha katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Hija kuwa “Mahujaji 1,070,000 wamewasili katika Ufalme kufikia Jumapili.” Idadi hii inatarajiwa kuongezeka kadri Mahujaji zaidi wanavyoendelea kuwasili katika maeneo matukufu katika siku zijazo.

Kila mwaka, mamilioni ya Waislamu kutoka pembe zote za dunia hukusanyika Makkah kutekeleza ibada ya Hija, ambayo ni safu ya ibada zinazotekelezwa kwa siku kadhaa na hubeba uzito mkubwa wa kiroho kwa Waislamu.

Hija hufanyika kila mwaka katika mwezi wa Dhul-Hijjah wa kalenda ya Kiislamu ya mwezi. Ibada ya Hija huanza rasmi tarehe 8 ya mwezi huo na hukamilika tarehe 13. Mwaka huu, Hija inatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 4 hadi Juni 9, 2025, ingawa tarehe kamili zitatangazwa rasmi kulingana na kuandama kwa mwezi.

Maafisa wa Saudi Arabia wamewasihi Waislamu wa maeneo ya ndani kutazama anga siku ya Jumanne kwa ajili ya kuona mwezi mwandamo utakaothibitisha kuanza kwa mwezi wa Dhul-Hijjah. Uthibitisho wa mwezi huu mpya ni muhimu ili kuamua rasmi tarehe ya kuanza kwa Hija na pia siku ya Idd al-Adh’ha, inayoadhimishwa siku ya 10 ya Dhul-Hijjah.

Idd al-Adh’ha, au “Sikukuu ya Kuchinja,” ni mojawapo ya sikukuu kuu mbili za Kiislamu. Inaadhimisha utiifu wa Nabii Ibrahim (AS) alipojitoa kumchinja mwanawe kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu. Sikukuu hii huadhimishwa kwa swala ya pamoja, kutoa sadaka, na kuchinja wanyama kama vile kondoo, ambapo sehemu ya nyama hugawiwa kwa watu wenye uhitaji.

3493242

Kishikizo: hija saudi arabia
captcha