IQNA

Msomi wa Lebanon: Fikra za Imam Khomeini zinategemea Qur’ani

21:15 - June 04, 2025
Habari ID: 3480787
IQNA – Mtaalamu mmoja kutoka Lebanon amesema kuwa lengo la harakati ya Imam Khomeini ilikuwa kuelekea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na hivyo fikra zake zikitokana na misingi ya Qur’ani Tukufu.

Bi Linda Taboush, mhadhiri wa chuo kikuu na mchambuzi kutoka Lebanon, alitoa kauli hiyo alipohutubia katika warsha ya mtandaoni yenye kichwa cha habari “Imam Khomeini (RA): Mfano wa Kuigwa wa Mabadiliko Katika Ulimwengu wa Kiislamu”, iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Habari za Qur’ani (IQNA) Jumanne hii kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema kuwa Imam Khomeini aliendeleza harakati ya Ashura, akaliongoza mapinduzi makubwa zaidi ya zama hizi hadi ushindi, na kuasisi mfumo wa kiutawala uliokuwa na nguvu zaidi katika enzi ya kisasa.

Amesisitiza kuwa Imam Khomeini hakuwa mtu wa mabavu, au udikteta; bali alikuwa shakhsia adhimu, mwenye taqwa na ucha Mungu. “Silaha zake zilikuwa ni khofu ya Mwenyezi Mungu, ucha Mungu na ukweli wa maneno yake. Na ni kwa misingi hiyo ndiyo sisi watu wa Lebanon tumelelewa na kufundishwa,” amesema.

Aidha, Bi Taboush amesema kuwa Imam Khomeini alikuwa na roho tukufu na haiba ya kipekee ambayo ilimuwezesha kuchukua uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wakati huo na kuikomboa Iran kutoka katika makucha ya mabeberu kwa kauli mbiu ya uadilifu, maendeleo na uhuru,  na hatimaye kuokoa ubinadamu kutoka kwenye giza la ujinga na upotofu.

Ameongeza kuwa Imam Khomeini alikuwa mtu wa kwanza kuutaja utawala wa Kizayuni kuwa ni “uvimbe wa saratani” na kusisitiza haja ya kuondolewa kwa uvimbe huo.

Kigezo cha uongozi kwa Imam Khomeini kilikuwa ni hekima na utambuzi wa hali, na kutokana na uongozi wake wa kimungu na wenye busara, Harakati ya Uamsho wa Kiislamu iliweza kuundwa kwa misingi maalum, kanuni thabiti na sifa bainifu hadi katika pembe za mbali za dunia, kwa lengo la kuzuia ubeberu na utawala wa Marekani na Uzayuni, pamoja na kuangamiza harakati za ubaguzi wa rangi ndani ya Iran na katika mhimili wa muqawama.

Mhimili huo wa muqawama, ambao nguzo yake kuu alikuwa shahidi mkuu Sayyid Hassan Nasrallah, umeendelea kuwa imara na thabiti kwa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa mwongozo wa Kiongozi wa Mapinduzi, Imam Khamenei, amesema Taboush.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, amesisitiza msimamo wa Imam Khomeini kuhusu kueneza Uislamu wa kweli wa Mtume Muhammad (SAW) na Qur’ani, kuimarishwa kwa dhana za umoja wa Kiislamu pamoja na misingi na maudhui msingi ya ibada ya Hija.

Ayatullah Ruhollah Moussavi Khomeini, anayefahamika zaidi kama Imam Khomeini, ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 nchini Iran, yaliyopelekea kuangushwa kwa utawala wa Shah wa Iran aliyekuwa kibaraka wa Marekani.

Alizaliwa mwaka 1902 na akawa kiongozi mashuhuri wa harakati ya taifa la Iran dhidi ya udikteta wa kifalme uliodumu kwa karne nyingi. Imam Khomeini alifariki dunia na kurejea kwa Mola wake tarehe 3 Juni, mwaka 1989 akiwa na umri wa miaka 87.

/3493324

Habari zinazohusiana
Kishikizo: lebanon imam khomeini
captcha