Akizungumza jijini Tehran katika mkesha wa kumbukumbu ya mwaka wa 36 tokea alipoaga dunia Imam Khomeini, Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Pezeshkian amebaini kuwa Imam Khomeini alihimiza uhuru, heshima na kusimama kidete, akiongeza kuwa mahasimu wa Jamhuri ya Kiislamu wanadhani wanaweza kuzima maendeleo ya nchi za Kiislamu katika nyanja za sayansi na ubunifu kupitia vitisho na rushwa , lakini jitihada zao hazitazaa matunda.
Rais wa Iran amesema: “Wapinzani wa nje pamoja na vibaraka wao wa ndani wanatumia mabilioni ya dola na kampeni za propaganda ili kuathiri mshikamano wa kitaifa kwa kusambaza uvumi na uongo."
“ Marekani, utawala wa Israel na washirika wao wanachochea mifarakano na machafuko ili kufanikisha ajenda zao ovu. Hata hivyo, hawatofanikiwa kamwe kuuvunja umoja wa taifa la Iran.”
Kuhusu sera za kigeni, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran inatamani amani na usalama, na haijawahi wala haitafuti kumiliki silaha za nyuklia.
“Wale wanaodai kuwa Iran inatafuta silaha za maangamizi ni haohao wanaotishia Waislamu katika eneo hili kwa silaha hizo hizo,” alisema. Akaongeza, “Hakuna mtu mwenye dhamiri safi na anayetafuta uhuru anayeweza kufumbia macho ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni kwa msaada wa Marekani na Ulaya.”
Imam Khomeini aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake akiwa na umri wa miaka 86 mnamo tarehe 3 Juni 1989. Anahesabiwa kama mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi katika historia ya kisasa, baada ya kuongoza vuguvugu la wananchi dhidi ya utawala wa kifalme wa Pahlavi, ambao ulikuwa kibaraka na mshirika wa karibu wa Marekani.
Mamilioni ya Wairani kutoka kila tabaka la kijamii, pamoja na idadi kubwa ya Waislamu pamoja na wapenda uhuru duniani kote, wameadhimisha kumbukumbu ya miaka 36 tangu kuaga dunia kwa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Ruhollah Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu).
Hafla kuu ya maombolezo ilifanyika katika Haram ya Imam Khomeini kusini mwa Tehran, siku ya Jumatano, ambapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, alihutubia halaiki kubwa ya waombolezaji.
Maombolezo ya mwaka huu, yaliyoandaliwa chini ya kaulimbiu "Imam wa Matumaini na Nguvu", kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, yalivuta maelfu ya wafanyaziara katika eneo la kaburi la Imam Khomeini, huku matukio kama hayo yakifanyika katika mamia ya miji na vijiji kote nchini Iran.
Waislamu na wafuasi wa Imam Khomeini katika mataifa mbalimbali pia waliandaa hafla za maombolezo, ikiwemo katika nchi za Asia Magharibi, Afrika, na hata barani Ulaya.
Imam Khomeini alitumia miaka mingi uhamishoni katika nchi kama Iraq, Uturuki na Ufaransa, akiwaongoza wafuasi wake kupitia harakati ya wananchi ambayo hatimaye iliufuta utawala wa kifalme uliodumu kwa maelfu ya miaka nchini Iran.
Kumbukumbu hii ya mwaka pia inatangulia siku nyingine muhimu ya kihistoria—tarehe 5 Juni 1963—ambayo inahesabiwa kuwa siku ya mwanzo wa mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa kifalme, ambapo maandamano makubwa yalifanyika mjini Tehran na Qom.
4286221