Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, CAIR, shirika kubwa zaidi la kutetea haki za kiraia za Waislamu nchini Marekani , limesema kuwa Fine ameendelea kutumia “kauli zenye misingi ya chuki dhidi ya Uislamu na dhana potofu dhidi ya Wapalestina,” huku akihamasisha “ghasia dhidi ya Waislamu na Wapalestina, ndani na nje ya Marekani, bila kuchukuliwa hatua yoyote.”
Uamuzi huo wa kumtaja umetolewa kufuatia msururu wa matamshi ya hadharani ya mbunge huyo wa Florida, ikiwemo kauli tata aliyoitoa katika runinga ya taifa mwezi Mei 2025, ambapo alipendekeza Marekani kufikiria kutumia silaha za nyuklia dhidi ya Gaza, akilinganisha hali hiyo na mabomu ya atomiki yaliyotumika dhidi ya Japani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Alipotakiwa kufafanua, Fine alisisitiza msimamo wake kwa kauli ambazo CAIR imezitaja kuwa za kibaguzi na zinazodhalilisha utu.
Kwa mujibu wa CAIR, Fine alidai kuwa “nusu ya wakazi wa Gaza wameoana na ndugu zao wa karibu na wana matatizo ya akili,” na alipuuzilia mbali ukosoaji dhidi ya kauli yake.
Licha ya uzito wa matamshi hayo, CAIR imesema kuwa hadi sasa hakujakuwa na hatua ya kumlaumu wala kumkemea hadharani kutoka kwa uongozi wa chama cha Republican. Shirika hilo limeongeza shinikizo kwa Bunge la Marekani kumwadhibu rasmi Fine, hasa baada ya kutoa tena kauli zinazodhalilisha Wapalestina wiki iliyopita.
Mnamo Aprili, CAIR ilisambaza barua kwa wanachama wote wa Bunge la Marekani pamoja na wafanyakazi wa ofisi zaidi ya 1,600 wa bunge, ikiwataka wabunge kupinga kile ilichokiita “matamshi hatarishi dhidi ya Waislamu, Wapalestina, na maadili ya Marekani.”
Kundi hilo pia limeangazia matukio ya awali yanayomhusisha Fine, yakiwemo machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii akitaka Gaza “iharibiwe,” kumuita mbunge mwenzake “gaidi Muislamu,” na kuonekana akicheka na picha ya mtoto wa Kipalestina aliyefariki. Aidha, Fine alimwambia mmoja wa wapiga kura wake Muislamu kwamba “nenda ukijilipue mwenyewe” na alilitaja vazi la Kipalestina keffiyeh kuwa ni “kitambaa cha magaidi” wakati wa kikao cha hadhara.
CAIR sasa inatoa wito kwa Spika wa Bunge Mike Johnson na Kiongozi wa Upinzani Hakeem Jeffries kuchukua hatua za wazi ikiwa ni pamoja na kumlaani rasmi mbunge huyo, kumuondoa kwenye kamati zote za bunge, na kuwahimiza wabunge wengine wasishirikiane naye
Shirika hilo limesema litaendelea kushirikiana na wanaharakati wa haki za kiraia na viongozi wa kisiasa kuhakikisha Mwakilishi Fine anawajibishwa ipasavyo.
3493416