Wakandarasi wanaojenga mtaa ambao wakaazi wake wengi aghalabu ni Waislamu karibu na Dallas wamekana madai ya ubaguzi kufuatia uzinduzi wa uchunguzi wa haki za kiraia wa serikali shirikisho kuhusu mradi huo.
Uchunguzi huo ulitangazwa Ijumaa na Seneta wa Marekani John Cornyn, ambaye awali alionyesha wasiwasi kwamba mradi huo unaweza kuwanyima Wakristo na Wayahudi haki ya kuishi katika mtaa huo.
Mradi huo, uitwao EPIC City, ni jamii ya mchanganyiko inayohusishwa na Kituo cha Kiislamu cha East Plano (EPIC), ambacho hakijajengwa bado. Wakandarasi wanasema kuwa mpango huo unajikita katika uhuru wa dini na ujumuishi, na wamesema kwamba unalengwa visivyo kwa sababu ya uhusiano wake na Uislamu.
Seneta Cornyn, Mrepublikan kutoka Texas, alifichua kwenye chapisho lake kwenye X (aliyejulikana zamani kama Twitter) kwamba Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Pam Bondi, alimjulisha kuhusu uamuzi wa Idara ya Haki za Kiraia kufungua uchunguzi wa haki za kiraia wa shirikisho. Cornyn alikuwa ametaka uchunguzi huo Aprili, akihofia kwamba mradio huo unaweza kufanya kazi kama kisiwa cha kidini kinachozuia watu wa imani zingine.
Wakandarasi, kupitia wakili wao Dan Cogdell, walikana madai hayo kama yasiyo na msingi na yenye nia za kisiasa. Cogdell alisisitiza kwamba EPIC City inazingatia kikamilifu sheria na akawalaumu maafisa wa serikali kwa kulenga mradi huu kwa sababu ya utambulisho wake wa Kiislamu.
"Shambulio dhidi ya mradi huu kuhusu sheria za Kiislamu na madai mengine si tu kwamba hayana msingi wowote bali pia yanapotosha na ni hatari pia," alisema Cogdell Ijumaa.
Cogdell aliongeza kusema kuwa hakungekuwa na uchunguzi wa aina hii kama mradi ungekuwa umeunganishwa na kanisa au sinagogi.
Maafisa wa serikali, ikiwa ni pamoja na Gavana Greg Abbott wa Republican na Mwanasheria Mkuu Paxton — ambaye anapanga kugombea kiti cha Seneti mwaka 2026 dhidi ya Cornyn — pia wameanzisha uchunguzi kuhusu EPIC City. Hii ni pamoja na maswali kuhusu uvunjaji wa kanuni za kifedha, sheria za makazi ya haki, na madai kwamba msikiti uliohusika unaweza kuwa umefanya huduma za mazishi bila ruhusa.
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Amerika (CAIR) huko Dallas limekosoa vikali hatua za serikali na shirikisho, likiziita kama unyanyasaji unaokiuka katiba. Baraza hilo ambalo hutetea haki za Waislamu limesisitiza kwamba uchunguzi huu unakiuka haki za wakandarasi za kujieleza kidini na ni aina ya kubughudhi inayofadhiliwa na serikali dhidi ya jamii ya Kiislamu.
Mpango wa EPIC City unajumuisha vitengo zaidi ya 1,000 vya makazi, shule za msingi na sekondari zinazotegemea mafunzo ya Kiislamu, chuo cha jamii, vituo vya huduma kwa wazee, na viwanja vya michezo. Eneo hili linapendekezwa karibu na mji wa Josephine, takriban maili 30 (kilomita 48) kaskazini-mashariki mwa Dallas.
3493015