IQNA

Mapinduzi ya Imam Hussein (AS) yalilenga kufufua roho na kiini cha Uislamu: Mwanazuoni wa Al-Azhar

17:40 - July 08, 2025
Habari ID: 3480914
IQNA – Mwanazuoni mmoja kutoka Misri amesema kuwa lengo la mapinduzi ya Imam Hussein (Aleyhi Salaam) lilikuwa kufufua roho na kiini halisi cha dini, wakati ambapo maadili na thamani sahihi za Kiislamu zilikuwa zimepotea, na kilichobakia ni maumbo ya nje tu ya ibada na mila za dini.

Sheikh Nadi al-Badri, profesa katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al-Azhar, alisema katika hotuba aliyotoa siku ya Ashura, siku ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), kuwa mapinduzi ya Imam Hussein (AS) yalikuwa ya kuhuisha dini ya kweli na kuwaita watu katika ibada ya Mwenyezi Mungu.

Ifuatayo ni tafsiri ya hotuba yake: Imepokewa kuwa mtu mmoja alimwambia Imam Hussein (AS): "Ewe ndugu yangu, wale walioko pamoja nasi watapata shahada. Lakini vipi kuhusu wale ambao hawako nasi?"

Imam Hussein (AS) akasema: "Watu hao hawajafikia uelewa wa maana ya dhana za juu. Ni Waislamu, lakini hawajafahamu maana ya Uimamu wala maana ya kujitolea muhanga kwa ajili ya dini ya Uislamu."

Kisha akasoma aya: "Inapokuja nusura ya Mwenyezi Mungu na ushindi." (Surah An-Nasr, aya ya 1)

Ushindi si tu kuishinda jeshi la makafiri wanaopigana na Waislamu na kuingia katika ardhi zao. Ikiwa pamoja na hilo, Mwenyezi Mungu hajafungua nyoyo zao kwa maadili ya Kiislamu, basi huo si ushindi wa kweli. Watu huona haya ni ushindi wa kijeshi, lakini si ushindi wa roho.

Imam Hussein (AS) akasema: "Yeyote ambaye hatuelewi, basi hajafahamu maana ya ushindi. Hajafaidika na kujua haki ya kujitolea na kujitoa mhanga kwa ajili ya dini na maadili ya Kiislamu. Huu ndio msingi aliouweka Mtume Mtukufu (SAW).

Wakati washirikina wa Quraysh walipomjia Mtume (SAW) na kumwambia aache wito wake, wakamwahidi mali, utawala, na heshima, wakasema: "Tutakujengea kasri bora kuliko wafalme wa Uajemi na Warumi."

Lakini Mtume (SAW) akasema: "Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hata mkiweka jua mkononi mwangu wa kulia na mwezi mkononi mwangu wa kushoto ili niache wito huu, sitauacha mpaka Mwenyezi Mungu auifanikishe dini hii au nife katika kuipigania."

Lengo kuu la Imam Hussein (AS) katika mapambano yake lilikuwa kuidhihirisha dini ya Mwenyezi Mungu – dini ambayo utukufu wake ulikuwa umetupiliwa mbali na watu kuanza kuwaabudu binaadamu na mali zao. Watu walikuwa wanaabudu dhahabu ya Bani Umayya na cheo na madaraka yao.

Mmoja alitaka utawala wa Rey, mwingine alitaka utawala wa Basra, mwingine alililia Khorasan, mwingine Transoxiana, na mwingine Misri. Watu walikuwa wanauza dini yao, maadili yao, na thamani zao kwa maslahi ya dunia. Dini ilikuwa ni ya nje tu; haikuwa tena na roho. Adhana ilipigwa lakini haikuwa na maana ya ndani. Waumini walikuwa mbali na kiini cha Swala. Lakini alibakia mmoja – aliyeushika mkataba wake na Mwenyezi Mungu.

Roho ya Uislamu haikuonekana tena katika ibada, maisha, na dhamiri za Waislamu.

Kwa sababu hiyo, bwana wetu Imam Hussein (AS) alisimama kupigania haki, kuwaongoza watu kutoka katika kuwaabudu wanadamu hadi kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee – kama alivyofundisha babu yake Mtume Muhammad (SAW) – kutoka gizani hadi kwenye nuru.

Imam Hussein (AS) alisema: "Nimesimama kwa ajili ya kufanya islah katika umma wa babu yangu. Kufufua amri ya mema (amr bil ma’ruf) na kukataza mabaya (nahy anil munkar). Sikusimama kwa ajili ya uasi, wala kwa ajili ya mali au mamlaka, wala kwa uovu au dhulma."

Bwana wetu Imam Hussein (AS) alisimama kwa ajili ya lengo hili – kuusimamisha ukweli na kuupinga batili.

3493739

Habari zinazohusiana
captcha