Mkutano wa 8 wa Kimataifa wa Arbaeen wafanyika Karbala
IQNA – Mkutano wa nane wa Kimataifa wa Matemberzi ya Arbaeen umefanyika Karbala, Iraq na wanazuoni kutoka nchi 35 wamejadili ufahamu wao kuhusu tukio hilo ambalo mwaka huu limewaleta Pamoja wafanyaziara milioni 21.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Karbala, lilihudhuriwa na shakhsia wa kidini, wanazuoni, wanajumuiya mbalimbali, watafiti na wanasiasakutoka sehemu mbalimbali za dunia, kwa mujibu wa kituo cha habari cha Imam Hussein (AS).
Abdulamir Aziz Al-Quraishi Mkuu wa Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Karbala alihutubu kuhusu masuala mbalimbali ya hafla ya Ashura wakati wa kongamano hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Khatam Al-Anbiya katika Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS).
Amesema kuwa harakati ya Karbala haikuwa tu mapinduzi dhidi ya dhulma bali pia ni "harakati ya kina ya elimu" yenye thamani kubwa za kielimu, kimaadili na kimaadili zilizowekwa na Imam Hussein (AS) kwa kujitolea mhanga na kusimama kidete.
Al-Quraishi alielezea mwamko wa Imam Hussein (AS) kuwa "usio na kifani," akieleza kwamba uliunda historia mpya miongoni mwa Waislamu. "Kwa mara ya kwanza, mwamko ulianzishwa si kwa ajili ya madaraka au mali bali kwa ajili ya utu, heshima na ulinzi wa jamii."
Harakati ya Imam Hussein (AS) inadhihirisha thamani za juu kabisa za kibinadamu, zinazopita maslahi binafsi na malengo ya kidhalimu, na ilianzishwa kwa ajili ya kutetea misingi na uadilifu wa binadamu, alisema na kuongeza kuwa, harakati hiyo inasalia kuwa kielelezo mashuhuri cha mapambano ya utu wa mwanadamu.
Hassan Rashid Al-Abayji, Katibu Mkuu wa Haram Takatifu ya Imam Hussein (AS) ameashiria kuwa, suala la Palestina ni muendelezo wa mapambano au muqawama wa Imam Hussein (AS) akisisitiza umuhimu wa kusimama kwa haki na kuwaunga mkono wanyonge.
Ameongeza kuwa, harakati ya Imam Hussein (AS) imebakia hai kwa sababu ilisimama dhidi ya batili na kukataa unyonge na kujidhalilisha.
"Damu ilishinda upanga," alisema, na kuongeza, "Harakati ya Imam ilihakikisha kuwa Uislamu unabakia hai."
Amesisitiza kuwa, ibada ya ziara na matembezi ya Arbaeen huakisi baadhi ya picha za huzuni za dhulma inayowakabili Ahul Bayt au familia ya Mtume Muhammad (SAW).
Mkutano wa nane wa Kimataifa wa Matembezi ya Arbaeen, wenye mada "Ziara ya Arbaeen: Kuelekea Mifumo ya Ulimwenguni wa Ubinadamu na Ustaarabu," ulihitimishwa Alhamisi, Agosti 29.
Tukio hilo la siku mbili lilikuwa na mawasilisho na hotuba za wasomi kutoka nchi 36, kutia ndani Iraq, India, Malaysia, Italia, Uholanzi, Kosovo, Ireland, Bahrain, Tunisia, Ujerumani, Ubelgiji, Japan, Lebanon, na Iran.
Jumla ya makala 148 za utafiti ziliwasilishwa kwa sekretarieti ya mkutano, ambapo 100 zilikubaliwa baada ya uhakiki wa kitaalamu.