IQNA

Arbaeen ni fursa ya kuonesha ustaarabu mpya wa Kiislamu

18:45 - July 18, 2025
Habari ID: 3480963
IQNA – Afisa mmoja wa masuala ya utamaduni kutoka Iran amesema kwamba matembezi makubwa ya kila mwaka ya Arbaeen ni fursa ya kipekee ya kuonesha ustaarabu mpya wa Kiislamu.

“Arbaeen ni nafasi ya kipekee ya kuonesha ustaarabu mpya wa Kiislamu na njia ya haki wa Ahlul-Bayt (AS),” alisema Reza Moamemi Moghaddam, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni katika Taasisi ya Wakfu na Misaada ya Iran, katika mahojiano na IQNA kabla ya matembezi  ya Arbaeen ya mwaka huu.

Akinukuu maneno ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kuhusu Arbaeen, alisema kuwa Kiongozi huyo ameitaja Arbaeen kuwa ni njia kuu ya kuwasilisha ujumbe wa Uislamu; njia ambayo inavuka mipaka ya kijiografia, kikabila na kilugha, na kuunganisha nyoyo kwa upendo kwa Imam Hussein (AS).

Moamemi Moghaddam alisisitiza kuwa pale mamilioni ya watu wanapotembea pamoja kwa upendo, unyenyekevu, na kujitolea wakati wa Arbaeen, hiyo ni sura halisi ya utangulizi wa jamii ya Mahdawi (Jamii ya Imam Al-Mahdi aliyeahidiwa kuwa atarejea).

“Arbaeen ni mazoezi ya pamoja ya Ummah wa Kiislamu duniani kote kwa ajili ya maandalizi ya kuja kwa Imam Mahdi ambaye ni Mwokozi (na Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake),” alieleza.

Akaendelea kusema kuwa dunia ya leo inahitaji kusikia ujumbe wa Imam Hussein (AS), na ni jukumu la waumini kuufikisha ujumbe huo kwa walimwengu.

Arbaeen ni tukio la kidini ambalo aghalabu huadhimishwa  na Waislamu wa madhehebu ya Shia na wapenda uhuru kote duniani katika siku ya arubaini baada ya Ashura, siku ya kukumbuka kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa Kishia.

Ni moja ya mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini duniani unaowakusanya mamilioni ya Waislamu wa Kishia, pamoja na Waislamu wa Kisunni na hata wafuasi wa dini nyingine, ambao hufanya matembezi hadi Karbala, kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani na maeneo mengine duanini.

Mwaka huu, siku ya Arbaeen itasadifu tarehe 14 Agosti, na takriban Wairani milioni 4 wanatarajiwa kushiriki katika matembezi haya matukufu.

3493884

captcha