IQNA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa afika Misri, adai nchi yake inauheshimu Uislamu

20:06 - November 09, 2020
Habari ID: 3473343
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amedai kuwa Paris inaheshimu dini ya Uislamu na kwamba Waislamu ni sehemu ya jamii ya Ufaransa.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa anaendelea kufanya jitihada za kupunguza hasira za Waislamu duniani wanaoiandama nchi hiyo baada ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW

Katika mkondo huo, Jean-Yves Le Drian amedai kuwa Paris inaheshimu dini ya Uislamu na kwamba Waislamu ni sehemu ya jamii ya Ufaransa.  

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa amesema hayo jana mjini Cairo katika mazungumzo yake na mwenzake wa Misri, Sameh Shoukry. Le Drian ameongeza kuwa, kampeni iliyoanzishwa ya kususiwa bidhaa za Ufaransa katika mataifa ya Kiislamu haiwafai wale walioianzisha. 

Katika jitihada hizo za kutaka kupunguza hasira za Waislamu pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri na Sheikh Mkuu wa al Azhar, Ahmed al-Tayeb, ambayo ndiyo mamlaka ya juu zaidi ya kidini nchini Misri. 

Mazungumzo na harakati hizo za Paris zinakuja baada ya jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo kuchapisha tena katuni zinazomtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW, na baada ya matamshi yaliyotolewa na Rais Emmanue Macron wa Ufaransa akitetea matusi na uovu huo. Macron pia alisisitiza kuwa Ufaransa utaendelea kuchapicha vibonzo hivyo katika kile alichodai kuwa ni uhuru wa kujieleza!  

Matamshi hayo ya Rais wa Ufaransa yamechochea malalamiko na maandamano katika nchi nyingi za Kiislamu ambako jumuiya mbalimbali zinatoa wito wa kusisiwa bidhaa za Ufaransa.

Ripoti zinasema hadi sasa makampuni mengi yamesitisha kuuza na kunuunua bidhaa kutoka Ufaransa yakiitikia wito wa kususiwa nchi hiyo kama njia ya kumtetea Mtume wa Mwenyezi Mungu na matukufu ya Kiislamu.  

/3473069

captcha