IQNA

Mwanazuoni: Wiki ya Umoja wa Kiislamu iwe Harakati Dhidi ya Wapinzani wa Uislamu

17:57 - August 27, 2025
Habari ID: 3481143
IQNA – Msomi wa ngazi za juu wa Kiislamu Iran ametoa wito wa kufanya Wiki ya Umoja wa Kiislamu mwaka huu kuwa harakati kamili dhidi ya wapinzani wa Uislamu.

Hujjatul Islam Mohammad Hassan Akhtari, mkuu wa Makao Makuu ya Kuuadhimisha Wiki ya Umoja wa Kiislamu na Miaka 1,500 ya Kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu, Muhammad (SAW), ametoa kauli hiyo katika mkutano wa tatu wa makao makuu uliofanyika Tehran Jumanne.

Wawakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mikoa ya Iran, viongozi wa madhehebu ya Sunni nchini, wakuu wa vituo vikuu vya Kiislamu nchini, na kundi la watu wenye ushawishi katika nyanja ya kukurubisha madhehebu za Kiislamu walihudhuria pia mkutano huo.

Akisisitiza umuhimu wa umoja wa Ummah ya Kiislamu katika hali ya sasa, Hujjatul Islam Akhtari amesema: “Mwaka huu, kutokana na matukio katika eneo, hasa hali ilivyo Palestina na Gaza, kuzingatia umoja, mshikamano, na uhamasishaji wa Ummah ya Kiislamu ni muhimu zaidi kuliko miaka ya awali.

“Kama tutafanikiwa kuonyesha harakati inayofaa katika jukwaa la kimataifa wakati wa Wiki ya Umoja mwaka huu, itakuwa hatua yenye thamani na endelevu.”

Kiongozi huyo wa dini amesisitiza kuwa ni muhimu harakati zote ziwe katika njia ya kueleza na kusambaza umoja wa Kiislamu ili kuundwa harakati kamili na zinazoratibiwa, na kuchukua hatua kubwa dhidi ya wapinzani wa Uislamu, matokeo yake ikiwa ni ushindi na wokovu wa watu waliodhulumiwa wa Palestina na Gaza.

Hujjatul Islam Akhtari amesisitiza utekelezaji bora wa programu za Wiki ya Umoja, akisema: “Mbali na Wiki ya Umoja, mashirika na taasisi zinapaswa kuwa na programu za mwaka mzima na kuzitekeleza katika wizara na taasisi zao.”

Ameongeza kuwa  taasisi za serikali na taasisi za kimataifa kama Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa, Shirika la Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu, na Wizara ya Mambo ya Nje tayari zimeanzisha hatua nzuri katika ngazi ya kimataifa, na maelekezo yametolewa kwa balozi na vituo vya utamaduni vya Iran katika nchi mbalimbali kufuata njia hii kwa ushirikiano mkubwa zaidi.

Alieleza matumaini kwamba kwa jitihada za taasisi, wanazuoni, na wananchi, “tunaweza kutoa suluhisho bora kufanikisha umoja wa Kiislamu na kupata mafanikio yenye thamani katika dunia ya Kiislamu.”

Siku ya 17 ya Rabi al-Awwal, inayosadifiana na Septemba 10 mwaka huu, inaaminika na Waislamu Shia kama kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), wakati Waislamu Sunni wanaamini kuwa siku ya 12 ya Rabi al-Awwal (Ijumaa, Septemba 5) ni kama siku ya kuzaliwa kwa Mtume wa Mwisho.

Kipindi kilichopo kati ya tarehe hizo mbili kilitangazwa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na hayati mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini, katika miaka ya 1980.

Sherehe hii mwaka huu inafanyika huku Waislamu katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa wakikabiliana na mashambulizi ya mauaji ya kimbari ya kigaidi yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala huo uliazisha vita vyake vya kikatili dhidi ya Gaza Oktoba 7, 2023. Zaidi ya Wapalestina 62,000, wengi wao wanawake na watoto, wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israeli dhidi ya Gaza. Pia kumekuwa na vifo vingi kutokana na njaa iliyosababishwa na kizuizi cha Israeli katika eneo la Palestina.

3494396

Habari zinazohusiana
captcha