IQNA

Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu kufanyika Oktoba

19:42 - August 30, 2021
Habari ID: 3474240
TEHRAN (IQNA) –Kongamano la 35 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu limepengwa kufanyika mwezi Oktoba kwa njia ya intaneti.

Hayo yamesema na Hujjatul Islam wal Muslimin Hamid Shahriari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madehebu za Kiislamu ambaye ameongeza kuwa, iwapo maambukizi ya COVID-19 yatakuwa yamepungua kwa kiwango kinachokubalika wakati huo, idadi ndogo ya wageni kutoka nchi za nje wataalikwa kuhudhiria kikao hicho mjini Tehran. Hatahivyo amesisitiza kuwa aghalabu ya waalikwa wa kongamano hilo watashiriki kwa njai ya intaneti wakiwa katika maeneo mbali mbali duniani.

Hujjatul Islam wal Muslimin Hamid Shahriari ameyasema hayo Jumapili mjini Tehran katika hafla ya kuzindia nembo ya kongamano hilo.

Akizungumza na mwandishi wa IQNA, amesema kongamano hilo litafanyika baina ya Oktoba 24-28 ambayo ni Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Amesema maudhui kuu katika kongamano la mwaka huu ni ‘Amani na Kuzuia Mifarakano’. Mwaka jana pia kongamano hilo la Umoja wa Kiislamu lilifanyika kwa njia ya intaneti.

Mkutano huo hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shiia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3993786

captcha