Akinukuu Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari Ijumaa kwamba, "Mamlaka za Israeli zinaendelea kukataa juhudi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa kufikia gavana wa Gaza na misaada muhimu."
Wakati huo huo, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Francesca Albanese ametoa wito wa kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, iwapo atazuru Poland, na kusema kuwa Warsaw lazima ifuate kanuni za haki za kimataifa.
Francesca Albanese alisema jana Ijumaa kuwa wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wanatakiwa kuwakamata watu ambao mahakama hiyo imetoa hati za kukamatwa kwao, na kuongeza kuwa: "Poland, ambayo ililaani kushindwa kwa Mongolia kumkamata Rais wa Russia, Vladimir Putin, inapaswa kumkamata Netanyahu, kwa sababu ubaguzi katika utekelezaji wa sheria unadhoofisha mfumo wa haki wa kimataifa."
Wakati huo wananchi wa Poland walifanya maandamano jana huko Warsaw wakipinga uamuzi wa serikali ya nchi hiyo kumpa kinga Netanyahu na kuzuia kukamatwa kwake.
Itakumbukwa kuwa, Novemba 21, 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu yenye makao yake The Hague huko Uholanzi ilitoa kibali cha kutiwa nguvuni Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wake wa vita, Yoav Gallant kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Israel imeua wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa
Kwingineko, Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa Israel imewaua takriban wafanyakazi 370 wa kutoa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, na kuonya kwamba mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wafanyakazi wa misaada, misafara na vituo mbalimbali yamezuia kwa kiasi kikubwa jitihada za kutoa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina linalozingirwa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kuwa wafanyakazi 369 wa misaada ya kibinadamu wameuawa huko Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel Oktoba 2023, na kumulika maafa na hali mbaya inayowakabili raia wa eneo hilo.
Katika taarifa yake ya kila wiki, OCHA imesema kwamba 263 kati ya waliouawa na Israel, walikuwa wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), na kutahadharisha juu ya changamoto kubwa zinazokabili jitihada za kibinadamu katika kanda hiyo.
Taarifa ya UNICEF kuhusu watoto
Wakati huo huo Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa la (UNICEF) umetangaza kuwa, kwa akali watoto 74 wameuawa shahidi huko Gaza katika siku saba za kwanza za mwaka huu mpya wa 2025 kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya jeshi la Israel.
Catherine Russell, mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, asema kuwa zaidi ya watoto milioni moja huko Gaza ambao hawawezi kuhimili joto la chini wanaishi katika mahema ya muda, akiongeza kuwa tangu Desemba 26 mwaka jana, watoto wanane wamekufa kutokana na hypothermia (joto la mwili kupungua) na baridi.
Alisema: "Tumekuwa tukionya kwa muda mrefu kwamba ukosefu wa makazi ya kutosha, ukosefu wa upatikanaji wa lishe na huduma za afya, hali mbaya ya afya, na sasa hali ya hewa ya baridi inahatarisha maisha ya watoto wote huko Gaza."
Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF aliendelea: Watoto na watoto wachanga huko Gaza wanakabiliwa na hali hatari za kiafya.
Shirika hilo lennya mfuungamano na Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena limetoa wito wa kuboreshwa mara moja kwa mazingira ya usalama, ikiwa ni pamoja na kupatiwa amani malori ya utoaji wa misaada ya kibinadamu ili wafanyakazi wa misaada waweze kufikia kwa usalama jamii wanazokusudia kuzihudumia.
3491406