IQNA

Jinai za Israel

Wanajeshi wa Israel wavamia waumini wa Kiislamu Karibu na Msikiti wa Al-Aqsa

18:17 - December 22, 2023
Habari ID: 3478072
IQNA – Mji wa Al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel Ijumaa umeshuhudia vikosi vya Israel vikitumia gesi ya kutoa machozi na nguvu ziada kuwatawanya waumini karibu na eneo la Msikiti wa Al-Aqsa huku watu wengi wakiugua kwa kuvuta gesi hiyo ya machozi.

Mapigano hayo yalizuka katika mtaa wa Wadi al-Joz, karibu na eneo hilo takatifu, ambapo waumini walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya Sala ya Ijumaa. Walizuiwa kuingia Msikiti wa Al-Aqsa kwa wiki ya 11 mfululizo kutokana na vikwazo vya utawala dhalimu wa Israel.

Vikosi vya utawala katili Israel pia viliwalenga waandishi wa habari waliokuwa wakiripoti tukio hilo, kuwashambulia na kuwaondoa katika eneo hilo. Video zinazosambaa mtandaoni zilionyesha wanajeshi wa Israel wakiwarushia mabomu ya machozi waumini waliokuwa wakielekea msikitini.

Ni waumini 12,000 pekee walioweza kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa, kutokana na vizuizi vilivyowekwa na utawala haramu wa Israel.

Vikosi vya utawala uvamizi wa Israel pia vilifunga milango ya msikiti na kuwanyima kuingia wale waliokuwa wakiishi nje ya Mji Mkongwe wa al-Quds.

Wanaharakati wameendelea kutoa wito kwa watu kukusanyika na kusali huko Al-Aqsa, licha ya juhudi za Israel za kutaka kukoloni na kubadilisha hadhi ya kihistoria na kidini ya eneo hilo takatifu. Katika miezi ya hivi karibuni, walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali wameingia mara kwa mara katika eneo hilo takatifu chini ya ulinzi wa majeshi ya Israel.

Msikiti wa Al-Aqsa ni eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu  baada ya Masjid al-Haram huko Makka na Masjid al-Nabawi huko Madina. Utawala wa Kizayuni unatekeleza njama ya muda mrefu ya kupora eneo hilo takatifu la Waislamu na mahala pake kujenga hekalu la Kizayuni.

3486514

Habari zinazohusiana
captcha