IQNA

Waziri wa Wakfu wa Algeria asisitiza uchapishaji sahihi wa Qur’ani Tukufu

15:29 - September 22, 2025
Habari ID: 3481267
IQNA – Waziri wa Wakfu na Masuala ya Dini wa Algeria amesisitiza umuhimu wa umakini mkubwa katika uchapishaji wa Qur’ani Tukufu.

Katika kikao na wajumbe wa Kamati ya Mapitio na Marekebisho ya Uchapishaji wa Qur’ani nchini humo, Bw. Youssef Belmahdi alieleza kuwa ni lazima kuzingatia usahihi wa kielimu katika kuipitia na kuirekebisha Qur’ani, kwa lengo la kuchapisha nakala timilifu zinazostahiki hadhi ya Neno la Wahyi.

Kwa mujibu wa tovuti ya Al-Ayyam, Belmahdi alitembelea kamati hiyo Jumamosi, tarehe 20 Septemba, na kuhudhuria kikao chake cha mara kwa mara kilichofanyika jijini Algiers.

Waziri huyo alitoa pongezi kwa juhudi za wajumbe wa kamati katika kuhudumia Qur’ani Tukufu, na akasisitiza jukumu lao kubwa la kuhakikisha kuwa nakala zinazochapishwa ni sahihi na hazina makosa.

Aidha, alieleza kuwa Algeria imekuwa ikijitahidi kwa muda mrefu kuandaa na kusambaza Qur’ani katika matoleo mbalimbali, jambo linalodhihirisha nafasi ya kihistoria na kitamaduni ya taifa hilo katika kuitumikia Qur’ani na kuieneza duniani kote.

Kamati ya Mapitio ya Uchapishaji wa Qur’ani ya Algeria ilianza tena shughuli zake miaka michache iliyopita kwa amri ya waziri wa Waqfu wa wakati huo, kufuatia kuchapishwa kwa baadhi ya nakala za Qur’ani zilizoonekana kuwa na makosa ya uchapaji.

Wajumbe wa kamati hiyo huteuliwa na waziri wa Wakfu, na ajenda yao kuu ni kuhakikisha kuwa Qur’ani inachapishwa kwa usahihi kamili bila dosari yoyote.

3494692

Kishikizo: qurani tukufu algeria
captcha