Wizara ya Masuala ya Kidini na Waqfu ya Algeria, kwa kushirikiana na Ofisi ya Utalii na Ufundi wa Mikono ya Mkoa wa Mascara, imeandaa msafara maalum wa kisomo cha Qur’ani Tukufu unaosafiri kutoka mji hadi mji. Mpango huu ulianza Ijumaa, Julai 11, ukiwa na kaulimbiu: “Nuru ya Qur’ani Tukufu Inatuongoza na Kumbukumbu ya Wana Huru Ni Ahadi Yetu”, kwa mujibu wa ripoti ya Al-Ittihad.
Kituo cha kwanza cha msafara huo kilikuwa Msikiti Mkuu wa Imam Muslim katika mji wa Mascara, ambako wasomaji mashuhuri wa Qur’ani kutoka Algeria kama Sheikh Abdelaziz Sahim, Sheikh Abdelkarim Belhassen, na Sheikh Abdelmonem Baroudi walisoma aya tukufu kwa mahadhi ya kuvutia.
Katika kipindi cha siku tatu, msafara huu unatarajiwa kutembelea na kuendesha matukio ya kisomo katika misikiti ya miji na vijiji mbalimbali, vikiwemo Mascara, El Kharroub, Ghriss, Tighenif, Oued Tagaia, Mohammadia, Froha, El Bordj, Ain Farès, na Bouhanifia.
Sheikh Ali Zenadra, mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini na Waqfu wa Mkoa wa Mascara, alisema kuwa wasomaji kumi wa Qur’ani kutoka sehemu mbalimbali za Algeria wanashiriki katika msafara huu, wakitoa kisomo chao katika misikiti watakayozuru.
Mbali na usomaji wa Qur’ani, shughuli mbalimbali za kidini pia zimepangwa, ikiwemo ibtihal (qaswida za dua na kasida), zitakazoshirikisha wanafunzi kutoka madrasa za Qur’ani na vituo vya dini vinavyojulikana kama zawiya.
Viongozi wa misikiti na maafisa wa idara ya kidini pia watawasilisha mihadhara na mafunzo juu ya fadhila za kuhifadhi na kusoma Qur’ani Tukufu, ili kuhamasisha jamii, hasa vijana, kupenda na kuenzi Kitabu hiki cha Allah.
Zenadra aliongeza kuwa programu itahitimishwa kwa hafla ya kidini katika Msikiti wa Uthman Ibn Affan mjini Mascara, ambapo wasomaji wote waliohusika pamoja na vijana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 walioko katika madrasa za Qur’ani za mkoa huo watatuzwa na kupewa heshima maalum.
3493830