IQNA

Pendekezo la ‘Fainali ya Mabingwa’ kwa Washindi wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani

13:01 - September 29, 2025
Habari ID: 3481300
IQNA – Ahmad Abolqassemi, Qari mashuhuri kutoka Iran, amesisitiza uwezo wa kipekee wa nchi hiyo katika uwanja wa usomaji wa Qur’ani Tukufu, akipendekeza kuandaliwa mashindano mapya ya kipekee ya “fainali ya mabingwa” kwa washindi wa mashindano ya kimataifa ya Qur’ani, yatakayofanyika nchini Iran.

Akizungumza na IQNA, Abolqassemi alisema wazo hilo linaweza kutekelezwa kupitia Taasisi ya Al al-Bayt (AS), akieleza kuwa kuandaa fainali ya mabingwa nchini Iran litakuwa jambo la kupongezwa sana.

Aliongeza kuwa ili kunufaika na uwezo wa wanaharakati wa Qur’ani, ni muhimu kwa wasomaji mashuhuri wa Qur’ani kujitathmini angalau mara moja kwa mwaka, ili kuchochea juhudi zaidi na kuendeleza maendeleo yao, na juhudi hizo ziwe hazina kwao.

“Uwezo wa kuandaa mashindano ya Qur’ani nchini mwetu si siri kwa yeyote. Nilipokuwa Mkurugenzi wa Radio ya Qur’ani, tulizindua mashindano ya Qur’ani kupitia redio kwa kutumia vifaa vya kawaida, na yalipokelewa vizuri na maelfu ya watu,” alisema.

Ustadh Abolqassemi alipendekeza mpango wa muda mrefu aliouhimiza kwa miaka mingi: “Badala ya kuwaalika wasomaji kutoka nchi mbalimbali wanaoshiriki mashindano ya kawaida, tunapaswa kuwaalika mabingwa tu na qari waliotwaa nafasi za juu katika mashindano ya kimataifa yenye heshima.”

Alisisitiza kuwa Taasisi ya Al al-Bayt (AS) mjini Qom ina uwezo wa kuandaa tukio hilo la kimataifa kwa upekee mkubwa katika miaka ijayo.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, Abolqassemi alitaja mafanikio ya vipindi vya Qur’ani vilivyotengenezwa kwa ajili ya umma, kama vile kipindi cha Mahfel kinachorushwa na IRIB, akisema: “Ninachokihofia ni kuwa idadi ya vituo vya elimu ya Qur’ani nchini mwetu haitoshi kuwapokea watu wanaotamani kuhudhuria madarasa ya Qur’ani baada ya vipindi hivyo kurushwa.”

“Tushirikiane sasa na kuunda mfumo wa kitaifa uliofungamana, ili kila mtu, popote alipo nchini Iran, aweze kupata darasa la Qur’ani lililo karibu na makazi au mahali pa kazi. Vinginevyo, fursa hii itageuka kuwa hali ya kutoridhika,” alionya.

Qari huyo mwandamizi pia alieleza mafanikio ya kipindi cha ‘Mahfel Setareha’ kinachorushwa na mtandao wa Pooya kwa watoto na vijana, akisema: “Matumizi ya mazingira yenye furaha na wahusika wa kuvutia katika vipindi vya Qur’ani vimeonyesha kuwa vinaweza kuwavutia watoto na hata watu wazima. Kuendeleza njia hii ni muhimu kwa mustakabali wa elimu ya Qur’ani. Hakika, baada ya vipindi vipya kurushwa, kutakuwa na mwamko mkubwa wa kujifunza Qur’ani, na lazima tuwe tayari kwa siku hiyo.”

Kipindi cha Mahfel kinajulikana kwa kuonyesha usomaji wa Qur’ani na kueneza mafundisho ya Kiislamu, na kinapendwa sana na watazamaji duniani kote. Kinapeperushwa kila siku kwenye chaneli ya 3 televisheni ya IRIB kabla ya jua kuzama katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, kikitoa faraja ya kiroho kwa wanaofunga wanapojiandaa kufuturu.

Kwa kuzingatia Qur’ani kama msingi wake, kipindi hiki hulenga kuimarisha muda mfupi wa mapumziko kwa wanaofunga kupitia mijadala yenye maarifa na usomaji wa kuvutia wa Qur’ani Tukufu.

4307378

 

Habari zinazohusiana
captcha