IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Rais wa Iran asema Waislamu hawatavumilia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

19:28 - June 30, 2023
Habari ID: 3477217
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Kuivunjia heshima Qur'ani ni kuvunjia heshima na kudunisha ubinadamu na thamani za Kiislamu, na jamii ya Kiislamu haitavumilia suala hilo.

Wiki mbili baada ya Mahakama ya Rufaa ya Uswidi au Sweden kuruhusu maandamano ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu, polisi ya nchi hiyo imetoa ruhusa ya maandamano hayo na siku ya Jumatano iliyopita Qur'ani Tukufu ilichomwa moto na kuvunjiwa heshima katika sikukuu ya Waislamu ya Idul-Adh'ha. Kitendo hicho kiovu kimelaaniwa vikali ya Waislamu kote duniani.  

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kulaani kitendo cha kudhalilishwa Qur'ani Tukufu nchini Sweden amesema: "Wafusi wote wa dini za Mwenyezi Mungu wamechukizwa na kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu, ambacho kwa hakika ni dharau kwa ubinadamu na thamani za Kiislamu; na jamii ya Kiislamu haitafumbia jicho uhalifu huo." 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Waislamu katika maeneo yote ya dunia wameeleza kuchukizwa kwao na uovu huo.

Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa, vitendo vya kubeza na kuvunjia heshima matakatifu vinafanywa na wale wanaodai kutetea uhuru wa kusema na uhuru wa maoni na kuongeza kuwa: Vijana wanapaswa kuelewa kuwa Wamagharibi wanapinga uhuru, na wanachofanya ni kuinua juu bango la eti kuunga mkono uhuru wa kusema na maoni.

Mataifa mengi ya Waislamu kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq, Saudi Arabia, Kuwait, Pakistan, Jordan na Uturuki yametoa taarifa za kulaani kitendo hicho cha kishenzi cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden.

Wakati huohuo, Morocco imemuita nyumbani Balozi wake kutoka Sweden, kulalamikia jinai hiyo ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden.

Aidha Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimelaani kitendo hicho dhidi ya Qur'ani Tukufu, na kusema kitendo hicho kimefanywa na watu wenye mfungamano na mrengo wa kulia wa Sweden na kwamba serikali ya Uswidi ni mshirika katika uhalifu huo.

4151385/

captcha