IQNA

Jinai za Israel

Wapalestina walaani kitendo cha Wazayuni kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu

17:37 - October 12, 2022
Habari ID: 3475919
TEHRAN (IQNA)-Katika muendelezo wa mpango wa chuki dhidi ya Uislamu, mara hii walowezi wa Kizayuni wamechoma moto nakala kadhaa za Qur'ani Tukufu huko katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel.

Nidal al-Jabari Mkurugenzi wa Idara ya Wakfu za Kiislamu katika mji wa al-Khalil amesema, walowezi wa Kizayuni wamechoma moto nakala kadhaa za kitabu kitukufu cha Qur'ani katika msikiti wa Qaytoun jirani na haram tukufu ya Nabii Ibrahim (as) katika eneo la kale la al-Khalil.

Vita dhidi ya Uislamu au chuki dhidi ya Uislamu zimekuwa zikiendeshwa kwa mbinu mbalimbali katika baadhi ya mataifa ya Magharibi na vilevile katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Ukweli wa mambo ni kuwa, kampeni za chuki dhidi ya Uislamu zimegeuzwa na kuwa sera thabiti za Magharibi kwa ajili ya kukabiliana na Uislamu asili na sahihi. Ili kufanikisha siasa hizo za majitaka, maadui wa Uislamu wamepanga na kuratibu senario mbalimbali.

Kuwahusisha Waislamu na operesheni za kigaidi au kuituhumu dini tukufu ya Kiislamu kwamba, eti inaunga mkono vitendo vya kikatili na utumiaji mabavu, kueneza maandiko, picha na taswira zinazoitusi na kuivunjia heshima dini ya Kiislamu na Mtume Muhhammad (saw) kama matukio ya vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume huko Ufaransa na kuyapatia silaha makundi yenye misimamo ya kuchupa mipaka ambayo kidhahiri yanaonekana kuwa ni ya Kiislamu na kutumia vibaya vyombo vya habari ni miongoni mwa mbinu chafu za chuki dhidi ya Uislamu ambazo zimekuwa zikikaririwa mara kwa mara katika ulimwengu wa Magharibi na huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kupunguza mvuto wa Uislamu miongoni mwa kizazi cha vijana na kupambana na mambo matukufu na thamani za Kiislamu ni mbinu nyingine chafu zinazotekelezwa katika kampeni za chuki dhidi ya Uislamu. Katika miaka ya hivi karibuni, chuki dhidi ya Uislamu zinaonekana kuongezeka pia huko Israel na viongozi wa Tel Aviv na walowezi wa Kiyahudi wakiwa na nia ya kusuma mbele gurudumu la mpango wao huo mchafu hawana mipaka yoyote katika hilo. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika hali ambayo licha ya kuwa kwa mujibu wa hati na nyaraka mbalimbali za kimataifa kuheshimu dini na wafuasi wake ni miongoni mwa misingi ya thabiti ambayo haipaswi kukiukwa katika sheria za kimataifa, lakini Wazayuni maghasibu wamekuwa wakivunjia heshima dini ya Uislamu, Waislamu na hata kitabu chao kitakatifu cha Qur'ani bila ya wasiwasi wowote.

Khidhr Adnan, mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Jihad al-Islami ya Palestina amesema katika majibu yake kwa hatua ya Wazayuni ya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu na kuchomwa moto nakala kadhaa za kitabu hicho kwamba: Jinai hii imelenga dini ya juu kabisa miongoni mwa dini za mbinguni.

Afisa huyu wa ngazi ya juu wa Jihad al-Islami amekosoa vikali kimya cha mataifa ya Magharibi na kueleza kuwa, kimya cha vinywa na ndimi za watu ambao daima wamekuwa wakibwabwaja na kupaza sauti ya uhuru wa kuabudu na filihali wamenyamazia kimya jinai hii chafu na hawajajitokeza kuilaani ni jambo la kusikitisha mno.

Kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu kunakwenda sambamba na siasa za kuuyahudisha mji wa Beitul-Muqaddas na miji mingine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu sambamba na jinai ambazo zimekuwa zikifanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina. Kwa hakika kuchoma moto Qur'ani Tukufu ni ithbati tosha kwamba, siasa na sera za utawala wa Kizayuni wa Israel zimejengeka juu ya misingi ya ubaguzi na kutoheshimu itikadi za wengine.

Abdul-Latif Al-Qanou, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametoa taarifa akikemea na kulaani kitendo cha kuchomwa Qur'ani Tukufu na kueleza kwamba, kitendo hicho ni jinai ambayo inapaswa kukabiliwa na majibu. Aidha amesema, kitendo hicho kinaonyesha kuwa, adui Mzayuni na walowezi wa Kizayuni wameazimia kuanzisha vita vya kidini.

Nukta muhimu zaidi ni kuwa, tukio la kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu liimefanyika katika hali ambayo, baadhi ya nchi za Kiislamu zimeanzisha au zimo mbioni kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel. Kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kunaonyesha kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel kinyume na madai mataifa yaliyofuata mkumbo huo, siyo tu kwamba, hatua hiyo haijawa na manufaa kwa upande wa amani, bali imeandaa mazingira zaidi ya kuvunjiwa heshima dini ya Kiislamu. Kuanzisha uhusano wa kawaida na Israel kunaweza kutambuliwa kama sehemu ya mpango mchafu wa chuki dhidi ya Uislamu.

3480803

captcha