IQNA

Teknolojia ya kisasa kudhibiti umati yaanzishwa Makkah kabla ya Hija

15:11 - May 25, 2025
Habari ID: 3480735
IQNA – Mfululizo wa mifumo ya kiteknolojia ya hali ya juu umetangazwa rasmi kwa ajili ya kuboresha usimamizi wa mahujaji katika Msikiti Mtakatifu wa Makkah kabla ya Hija ya mwaka 1446 Hijri (2025).

Katika hatua ya kihistoria inayoongozwa na Mamlaka Kuu ya Kusimamia Masuala ya Msikiti Mtakatifu wa Makkah na Msikiti wa Mtume jijini Madina, mtandao maalumu wa vitambuzi vilivyo ardhini na vifaa vya kusoma wanaoingia umetumiwa kwa ufanisi mkubwa ili kufuatilia na kuelekeza harakati za Mahujaji kwa usahihi wa hali ya juu.

Teknolojia hii inalenga kuongeza ufanisi wa kiutendaji wakati wa tukio kubwa la ibada linalokusanya mamilioni ya Waislamu kutoka pande zote za dunia.

Mfumo huu mpya unachanganya kamera za uangalizi zenye Akili Mnemba na uwezo wa kugundua mwendo, na hivyo kuruhusu uchunguzi wa papo kwa papo katika maeneo ya kuingia na kutoka.

Mfumo huu wa tabaka mbili haufuatilii tu mienendo ya Mahujaji, bali pia hutambua maeneo yenye msongamano mkubwa, na hivyo kuruhusu maamuzi ya haraka na yenye msingi madhubuti kwa ajili ya kudhibiti umati.

Uwekaji wa vifaa hivi umejikita hasa kwenye maeneo ya kuingilia na kutoka ya msikiti, pamoja na ghorofa za juu za eneo la Mataf (eneo linalozunguka Al-Kaaba) na sehemu ya Mas’a (njia kati ya Safa na Marwa), ambazo hupokea Mahujaji wengi wakati wa ibada za kilele za Hija.

Mfumo huu unaotegemea takwimu umewekwa ili kusaidia maamuzi yenye usahihi wa hali ya juu, kuruhusu viongozi wa usalama na huduma kuchukua hatua zinazofaa kwa usambazaji wa umati na kuepusha msongamano wakati wa saa za kilele.

Aidha, unatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa hatua za kiusalama, na hivyo kupunguza hatari za msongamano na ajali zinazoweza kutokea.

3493212

Habari zinazohusiana
Kishikizo: hija teknolojia
captcha