IQNA

Vikundi vya Usomaji Qur’an Katika Misikiti ya Misri Vimepokelewa Vyema

14:30 - November 23, 2025
Habari ID: 3481561
IQNA – Vikundi vya usomaji Qur’an katika misikiti ya Mkoa wa Kaskazini mwa Sinai, Misri, vimepokelewa kwa shangwe na raia wa Kimasri.

Misikiti ya Kaskazini mwa Sinai ilishuhudia mahudhurio makubwa ya raia na waumini Ijumaa, wakati wa vikundi vya usomaji Qur’anI vilivyofanyika.

Vipindi hivi hufanyika kila Ijumaa baada ya Sala ya Ijumaa na kuendelea hadi Sala ya Alasiri katika misikiti ya mkoa huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Awqaf ya Kaskazini mwa Sinai, vikundi vya usomaji Qur’ani hufanyika kila wiki kwa mujibu wa mpango wa Wizara ya Awqaf wa kuimarisha uelewa wa kidini na kusambaza usomaji sahihi na fasaha wa Qur’an.

Vimeandaliwa chini ya usimamizi wa Waziri wa Awqaf, Osama Al-Azhari, taarifa ilibainisha.

Akirejelea juhudi za maimamu wa misikiti kuandaa vikundi hivi, Mahmoud Marzouk, mkurugenzi wa Idara ya Awqaf ya Kaskazini mwa Sinai, alisema mapokezi ya shauku ya vikundi vya usomaji Qur’ani vinaonyesha hamu ya watu wa mkoa huu kuunganishwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Marzouk aliongeza kuwa idara yake imeanzisha mpango huu kwa kufuata msisitizo wa Waziri wa Awqaf wa Misri juu ya kufanikisha mikusanyiko ya baraka ya usomaji Qur’ani, kufufua utamaduni wa usomaji wa pamoja kwa usahihi, na kuunda fursa kwa wanajamii wote kuboresha usomaji wao.

Kwa mujibu wa ripoti, mikusanyiko hii maarufu ya usomaji Qur’ani ni miongoni mwa shughuli muhimu za kidini za Wizara ya Awqaf na huwapa washiriki nafasi ya kusikiliza usomaji sahihi na kurekebisha usomaji wao mbele ya wanazuoni mashuhuri na viongozi wa sala wenye utaalamu.

Mikusanyiko hii pia ina nafasi muhimu katika kuimarisha uelewa sahihi wa Qur’an na kutafakari juu ya maana ya aya za Kitabu Kitukufu.

3495487

Kishikizo: misri qurani tukufu
captcha