IQNA

Misri yaunda kamati ya kufuatilia utendaji wa makari wa Qur’ani

19:56 - December 02, 2025
Habari ID: 3481602
IQNA – Umoja wa Makari na Wahifadhi wa Qur’ani Tukufu nchini Misri umetangaza kuundwa kwa kamati maalum itakayoshughulikia ufuatiliaji wa utendaji wa makari na kushughulikia malalamiko yanayohusu usomaji wao.

Katika taarifa rasmi, umoja huo umeeleza kuwa kundi la viongozi wa umoja limechaguliwa kuwa wajumbe wa kamati hiyo, ambayo itahakikisha kufuata sheria zilizopitishwa katika shughuli za kitaaluma. Aidha, kamati hiyo itaunda mifumo ya ufuatiliaji chini ya usimamizi wa Wizara ya Awqaf ya Misri ili kufuatilia hali ya wanaokiuka masharti.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa Sheikh Muhammad Hashad, rais wa umoja, ndiye mwenyekiti wa kamati; huku Sheikh Mahmoud al-Khisht (makamu wa rais), Abdul Fattah Tarouti (katibu mkuu), Sheikh Muhammad Abdulmojoud Khalifa, Ahmed Abu Fayouz, Sheikh Taha Muhammad Numani (mshauri wa kiufundi wa umoja), na Sheikh Muhammad Salem Amer wakiwa miongoni mwa wajumbe wake.

Kamati hiyo itaendelea kufanya kazi chini ya usimamizi wa Waziri wa Awqaf, Osama al-Azhari, hadi marekebisho ya sheria ya umoja yatakapokamilika, ili kubainisha utaratibu wa shughuli za makari na kudhibiti ukiukaji wowote.

Lengo kuu la kamati hii ni kudhibiti makari wanaokosea, kufuatilia mchakato wa usomaji na kusimamia utendaji wa makari katika misikiti na vituo vya Qur’ani. Kipaumbele kimewekwa katika kuzingatia masharti ya Sharia na viwango vya kitaalamu ili kuhakikisha usomaji sahihi, wenye ubora wa juu, na kulinda haki za wasikilizaji dhidi ya makosa yanayoweza kuathiri usahihi wa Qur’ani Tukufu.

Kamati pia itasimamia makari wapya na wale waliobobea, na kutoa mapendekezo muhimu kwa umoja na Wizara ya Awqaf ili kuboresha mifumo ya kielimu na ya usimamizi kwa ajili ya kuinua kiwango cha usomaji wa Qur’ani kote nchini.

Ni vyema kutambua kuwa hivi karibuni makosa kadhaa yameonekana katika usomaji wa baadhi ya makari wa Misri, jambo lililosababisha ukosoaji mkubwa. Aidha, video ya usomaji wa Sheikh Ahmed Ahmed Nuaina, mmoja wa makari mashuhuri, ilisambazwa ikionyesha makosa mawili, na usomaji huo ukawasilishwa kwa umoja kwa ajili ya uchunguzi.

3495585
Kishikizo: qurani tukufu misri
captcha