IQNA

Kitabu Kipya Malaysia Chatoa Tafakuri za Dakika Mbili Kila Siku Kuhusu Qur’ani Tukufu

20:54 - December 06, 2025
Habari ID: 3481621
IQNA – Kitabu kipya chenye tafakuri fupi 365 za kila siku kuhusu Qur’ani kimezinduliwa mjini Petaling Jaya, Malaysia, siku ya Ijumaa.

Kitabu hicho, “365 Qur’an – Tafakuri za Dakika Mbili Kila Siku” kilichoandikwa na Mahani Zubedy, kinalenga kufanya maandiko matukufu ya Qur’ani Tukufu yawe rahisi kufikiwa na Wamalaysia wa makundi yote ya kijamii. Kimechapishwa na kampuni ya Zubedy Sdn Bhd na kina jumla ya tafakuri 365. Kila tafakuri huanza na aya teule ya Qur’ani Tukufu kisha ikifuatwa na maelezo rahisi na ya kiutendaji.

Mahani alisema msukumo wa kuandika umetokana moja kwa moja na aya za Qur’ani Tukufu akisisitiza kuwa si tafsiri ya kitaaluma. “Kila mara ninaposoma aya, hunishangaza. Aya hunipa msukumo na hunifanya nitafakari,” alisema. Aliongeza kuwa maandiko hayo ni jinsi kila aya inavyomgusa binafsi.

Uzinduzi rasmi wa kitabu hicho ulifanywa na Tunku Zain Al-Abidin Tuanku Muhriz. Mahani alieleza matumaini yake kuwa wasomaji watafahamu kuwa kuunganishwa na Qur’ani si jambo lililowekewa kikomo kwa kundi fulani pekee. “Wakati mwingine tunadhani dini lazima ikaribiwe kwa namna maalum, lakini kwangu mimi Qur’ani inaonyesha kuwa yeyote anaweza kuunganishwa na kupata msukumo,” alisema.

Kwa upande wake, Tunku Zain Al-Abidin alisema muundo wa kitabu hicho unawasaidia watu wenye shughuli nyingi kurejea imani yao. Alibainisha kuwa wengi katika sera za umma, taaluma au biashara huhisi kutengwa. “Muundo huu mfupi unaturuhusu kuingia moja kwa moja bila kelele na usumbufu wa mitandao ya kijamii,” alisema. Aliongeza kuwa aya zilizoteuliwa hutoa msukumo, hutuliza na hukumbusha wasomaji kuhusu lengo lao la maisha.

Alieleza kujiamini kuwa kitabu hicho kitawanufaisha Waislamu na wasio Waislamu pia. Kimeelezewa kama mwongozo wa kila siku wa kiutendaji na kinapatikana katika maduka ya vitabu vya MPH kote nchini Malaysia.

3495627

Habari zinazohusiana
Kishikizo: malaysia qurani tukufu
captcha