IQNA

Turathi

Maktaba ya Riyadh yatunza nakala adimu za Misahafu

20:18 - April 11, 2025
Habari ID: 3480524
IQNA-Maktaba ya Umma ya Mfalme Abdulaziz (KAPL) mjini Riyadh, Saudi Arabia, inahifadhi nakala 400 adimu za MIsahafu kutoka zama mbalimbali za Kiislamu ambapo  nyingi ni za kati ya karne ya 10 hadi 13 Hijria.

Mkusanyiko huu ni hazina ya sanaa ya Kiislamu, ukionyesha ustadi wa hati, mapambo ya dhahabu, usanifu wa kurasa, na ubunifu wa kipekee. Miongoni mwa nakala maarufu ni msahafu uliokunjwa wenye Aya ya Al-Kursiy, uliopambwa kwa mimea na kuandikwa kati ya fremu za dhahabu na kunakiliwa mwaka 1284 Hijria na Fakhr al-Din al-Suhrawardi.

Nakala nyingine ni msahafu wa kurasa 30, kila sehemu mbili zikiwa na sehemu kamili ya Qur'an. Kurasa zake zimepambwa kwa dhahabu na rangi ang’avu kwa mitindo ya mimea, na uliandikwa kwa khati ya Naskh mwaka 1240 Hijria (1824 Miladia).

Pia kuna msahafu mzima uliokamilishwa mjini Makka mwezi wa Ramadhani mwaka 1025 Hijria (1616 Miladia) na mwanazuoni mashuhuri Mulla Ali Al-Qari, uliopambwa kwa jedwali za rangi nyekundu na buluu. Nakala nyingine ya mwaka 920 Hijria (1514 Miladia) ina mapambo ya maua na maumbo ya jiometri, yote ndani ya paneli za dhahabu.

Msahafu mwingine wa kifalme umeandikwa kwa uangalifu mkubwa, umefungwa kwa ngozi iliyotiwa nta na mapambo ya dhahabu na maua. Kuna pia misahafu ya Andalusia, Maghreb, India, China, Kashmiri, na Mamluki — yote ikionyesha utofauti wa maandishi kama Kufic, Naskh, Thuluth, na maandishi ya Sudan, Levant, Iraq, Misri, Yemen, Najd na Hijaz.

Kila taifa la Kiislamu lilichangia kwa ubunifu wake wa rangi, mapambo na mtazamo wa kiutamaduni katika kunakili Kitabu Kitakatifu.

3492641

Habari zinazohusiana
captcha