CAIR, shirika kubwa zaidi la kutetea haki za Waislamu nchini Marekani, limetoa taarifa kali kulaani matamshi ya Maguire na kuitaka Sequoia Capital ikatize uhusiano wake naye.
Tukio hilo linatokana na chapisho la Maguire kwenye mtandao wa X wiki iliyopita, akimlenga Zohran Mamdani, mbunge wa jimbo la New York na mgombea wa nafasi ya umeya wa jiji hilo. Katika chapisho hilo, lililotazamwa zaidi ya mara milioni 5.5 hadi sasa, Maguire aliandika: “Mamdani anatoka katika tamaduni inayodanganya kila kitu. Ni kama sifa nzuri kudanganya ikiwa inasaidia ajenda yake ya Kiislamu.”
Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa Utafiti na Utetezi wa CAIR, Corey Saylor, alieleza chapisho hilo kama “ubaguzi wa wazi dhidi ya Waislamu.” Aliongeza: “Tunaamini kuwa viongozi wa Sequoia Capital wanachukizwa na chuki kama sisi. Tunatumai uongozi wa Sequoia utachukua msimamo dhidi ya uchochezi wa chuki na kumwondoa Maguire katika nafasi yake.”
Zahra Billoo, Mkurugenzi Mtendaji wa tawi la CAIR katika eneo la San Francisco Bay, alisema kuwa matamshi hayo si tu ya kuudhi bali pia ni hatari. “Yanarejea dhana potofu za chuki dhidi ya Uislamu ambazo kwa miongo kadhaa zimekuwa zikichochea unyanyasaji, ubaguzi, na mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini Marekani,” alisema. “Ikiwa kampuni hii inathamini usawa na ujumuishaji, lazima ichukue hatua madhubuti.”
Sequoia Capital, kampuni maarufu ya uwekezaji yenye miradi mikubwa kama Apple na YouTube, haijatoa tamko rasmi. Hata hivyo, zaidi ya waanzilishi 900 wa kampuni za teknolojia wamesaini barua ya wazi wakitaka Sequoia ilaani matamshi ya Maguire na kushughulikia “mtindo wa mara kwa mara wa chuki dhidi ya Waislamu.”
Ingawa Maguire alitoa video ya kuomba msamaha “kwa yeyote aliyeudhika,” hakujiondoa kwenye matamshi yake, jambo lililoibua ukosoaji zaidi.
Kiongozi wa muda mrefu wa sekta ya teknolojia ya Silicon Valley, Dilawar Syed, alieleza matamshi hayo kama “chuki dhidi ya Waislamu” na akaonya kuwa kauli kama hizo zinahatarisha ujumuishaji katika sekta ya ubunifu. “Tunahitaji kuhakikisha kuwa mazingira ya ubunifu yanajumuisha wote na hayana nafasi kwa kauli zinazodhalilisha jamii nzima,” alisema.
/3493792