IQNA

Kutoka Malaysia hadi Ulimwenguni: Mradi mkubwa wa kusambaza nakala za Qur'ani Tukufu

15:55 - February 20, 2026
Habari ID: 3481964
IQNA – Mpango mkubwa nchini Malaysia wa kusambaza nakala milioni moja za Qur'ani Tukufu kupitia mfumo wa waqf unakaribia kufikia lengo lake la mwisho kwa kasi kubwa.

Mradi wa Mshikamano wa Waqf wa Malaysia wa Misahafu Milioni Moja, uliopendekezwa kwa mara ya kwanza na Waziri Mkuu Anwar Ibrahim mwaka 2023, umefikia hatua ya juu ya utekelezaji, ambapo nakala 700,000 tayari zimechapishwa, huku nakala 300,000 zilizobaki zikiwa katika hatua ya uzalishaji.

Mwenyekiti Mtendaji wa Taasis ya Restu, Abdul Latiff Mirasa, alisema kuwa kundi la mwisho la Misahafu linatarajiwa kuwa tayari ndani ya miezi mitatu hadi minne ijayo.

Aliongeza kuwa zaidi ya nakala 500,000 tayari zimesambazwa ndani ya Malaysia na nje ya nchi, ikiwemo Afrika na Asia.

Mpango huu wa waqf wa wananchi unalenga kueneza mwito wa Kiislamu (da‘wah) na kuimarisha nafasi ya Malaysia kama kitovu cha kimataifa cha Qur’ani Tukufu.

“Mpango huu umekuwa na athari kubwa sana na umemwinua Waziri Mkuu kama balozi wa kimataifa wa Qur’ani. Kwa sasa, tunatuma kontena moja hadi mawili ya Qur’ani kwenda maeneo mbalimbali duniani karibu kila mwezi,” alisema.

Waziri Mkuu Anwar Ibrahim alitangaza mpango huu mwezi Januari 2023 kama jibu la busara na la Qur’ani dhidi ya matukio ya kuchomwa Qur’ani nchini Sweden, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kukuza uelewa bora wa ujumbe wa Qur’ani miongoni mwa dini na jamii tofauti.

Kuhusu juhudi za tarjuma, Abdul Latiff alisema kuwa mradi huo kwa sasa umefikia lugha 30, huku idhini ikitolewa kuongeza lugha nyingine 20 hadi 30 kwa awamu.

“Angalau lugha mpya 12 zinatarajiwa kukamilishwa mwaka huu, zikiwemo Kivietinamu, Kithai, Kilao, Kiiban, pamoja na Kiurdu na Kirusi,” alisema.

Hadi sasa, Taasisi ya Restu imetafsiri Qurani Tukufu katika lugha mbalimbali, zikiwemo Kimalay, Kiingereza, Kikmer, Kitagalogi, Kihispania (Ulaya na Amerika ya Kusini), Kifaransa, Kiitaliano, Kiswahili, Kihausa, Kireno, Kidenmark, Kiswidi, Kijerumani, Kichina (Mandarin), Kihindi, Kitamil, Kimalayalam, Kibosnia na Kiburma.

Takribani wataalamu 100 wanashiriki katika kazi ya tafsiri na urembo wa misahafu, huku toleo zote zikikaguliwa kwa umakini mkubwa kulingana na msingi wa maandishi ya Uthmani, yaliyoidhinishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Malaysia.

“Kila toleo la lugha huchukua kati ya miezi mitatu hadi sita kukamilika. Pia tunashirikiana na wataalamu kutoka Uturuki na Saudi Arabia ili kuhakikisha tafsiri zinakuwa sahihi na zinaendana na itikadi ya Ahl Sunnah wal Jamaah,” alifafanua.

Wakati huohuo, Abdul Latiff alibainisha kuwa Taasisi hiyo inaandaa Mushaf Malaysia Madani, unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi na Waziri Mkuu katika mwezi huu wa Ramadhani.

Mus’haf huo, ulioandikwa kwa mkono kwa muda wa miaka mitano, unachanganya kaligrafia ya jadi ya Kijawi ya Kimalay na teknolojia ya kisasa ya QR code, inayowawezesha wasomaji kusikiliza qira’a na kusoma tafsiri kupitia simu janja.

3496484

captcha