IQNA

Urithi wa Bingwa: DIHQA yamtaja Sheikh Al‑Hussary kuwa ‘Shakhsia wa Qur'ani Duniani’

14:08 - February 26, 2026
Habari ID: 3481998
IQNA — Zaidi ya miongo minne tangu kufariki kwake, sauti tulivu na yenye khushuu ya Sheikh Mahmoud Khalil Al‑Hussary bado inaendelea kuzunguka na kugusa nyoyo za Waislamu kote katika ulimwengu wa Kiislamu.

Sheikh huyo ametangazwa rasmi kuwa 'Shakhsia wa Qur'ani Duniani (Global Quranic Personality) katika toleo la 28 la Tuzo ya Kimataifa ya Qurani Tukufu ya Dubai (DIHQA), ikiwa ni heshima kubwa inayotambua mchango wake wa kipekee katika kuhudumia Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Tuzo hiyo inatambua elimu pana ya Sheikh Al‑Hussary kuhusu Qur'ani Tukufu, athari yake kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu, pamoja na mchango wake mashuhuri katika elimu ya Tajwidi na kuasisi madrasah ya kisasa ya qiraa ya Qur'ani.

Kupitia jukwaa la kijamii la X, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Falme za Kiarabu (UAE) na Mtawala wa Dubai, alieleza kuwa Sheikh Al‑Hussary alikuwa:

“miongoni mwa maqari wakubwa zaidi wa zama zetu… wa kwanza kurekodi murattal kamili ya Msahafu mzima, na mmoja wa wasomaji wa Qur'ani wanaofuatiliwa zaidi duniani.”

Aliongeza kuwa tuzo hiyo ya dola milioni moja itatangazwa rasmi katika hafla itakayofanyika tarehe 2 Machi, sambamba na kutangazwa kwa washindi wa tuzo ya dola milioni moja ya usomaji mzuri zaidi wa Qur'ani kwa wanaume na wanawake.

Sheikh Mohammed pia aliwahimiza watu kushiriki kupiga kura ya umma, ili kuchagua sauti bora zaidi miongoni mwa maqari sita wa kimataifa waliotajwa kuwa na sauti za kipekee za Qurani.

“Milango ya kura za umma sasa iko wazi ili watazamaji wachague Sauti Nzuri Zaidi ya Qur'ani kwa mwaka 2026,” aliandika.

 Madrasah ya kipekee ya Qiraa na umahiri wa kielimu

 Kwa upande wake, Ahmed Darwish Al Muhairi, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kiislamu na Shughuli za Kihisani Dubai (IACAD) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya DIHQA, alisema kuwa Sheikh Al‑Hussary aliasisi madrasah ya kipekee ya usomaji na umahiri wa Qurani, na akaweka misingi ya mbinu thabiti ya kielimu katika Tajwidi, ambayo vizazi duniani kote vimeendelea kunufaika nayo.

Sheikh Al‑Hussary alikuwa wa kwanza kurekodi Qur'ani iliyosomwa kwa kufuata kikamilifu kanuni za Tajwidi, na kurekodiwa rasmi kwa matumizi ya redio.

Alizaliwa tarehe 17 Septemba 1917 katika kijiji cha Shubra Al‑Namla, mkoani Gharbia nchini Misri. Alihifadhi Qurani Tukufu kabla ya kufikisha umri wa miaka minane, na baadaye akasoma Qiraa kumi katika Chuo Kikuu cha Al‑Azhar.

Mwaka 1957, aliteuliwa kuwa mkaguzi wa vituo vya usomaji Qur'ani nchini Misri, na baadaye akahudumu kama Kiongozi wa Maqari wa Misri na Mkuu wa Kamati ya Mapitio ya Msahafu.

Pia aliwahi kuwa Rais wa Muungano wa Dunia wa Maqari wa Qur'ani. Alikuwa msomaji wa kwanza wa Qurani kusoma katika Umoja wa Mataifa mwaka 1977, Kasri la Kifalme London mwaka 1978, na pia wa kwanza kusoma Qur'ani katika Ikulu ya White House na Bunge la Marekani.

Sheikh Al‑Hussary alikuwa na nafasi ya msingi katika kuanzishwa kwa redio ya kwanza ya Qurani duniani, na katika ukusanyaji wa sauti za Qurani. Sauti yake ndiyo ya kwanza kusikika kwenye Redio ya Qurani tarehe 25 Machi 1964.

Miongoni mwa vitabu na kazi zake mashuhuri ni:

  • Kanuni za Usomaji wa Qurani
  • Qiraa Kumi kutoka Al‑Shatibiyyah na Al‑Durrah
  • Mwongozo wa Waqfu na Ibtidaa
  • Urithi Bora katika Historia ya Maqari Kumi na Nne
  • Pamoja na Qurani Tukufu
  • Njia Mpya katika Elimu ya Tajwidi

Sheikh Mahmoud Khalil Al‑Hussary alifariki dunia tarehe 24 Novemba 1980, lakini urithi wake unaendelea kuishi katika masikio, nyoyo na midomo ya waumini hususan katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo Qur'ani husomwa kwa khushuu na unyenyekevu, kama alivyofundisha na kuacha mfano mwema kwa Umma wa Kiislamu.

 3496566

captcha