Katika ujumbe wake, Sheikh Akram al‑Kaabi amesema kuwa mhimili mzima wa Muqawama (Mapambano ya Kiislamu) uko tayari na unatii amri za Ayatullah Mojtaba Khamenei.
Ifuatayo ni sehemu ya ujumbe wa Sheikh Akram al‑Kaabi kwa Ayatullah Seyed Mojtaba Khamenei:
Ewe Ayatullahil Udhma Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei,
Tunamuomba Mwenyezi Mungu akujalie malipo makubwa kwa kuuawa shahidi shujaa wa Uislamu, kiongozi mwenye hekima na Sayyid mtukufu (Mwenyezi Mungu autakase moyo wake) , pamoja na mashahidi wote wa Mhimili wa Muqawama, hususan watoto wa shule wasio na hatia, na pia kwa mama yako mtukufu, mke wako mwema, dada yako mwenye heshima na mumewe, pamoja na watoto wao wawili wadogo.
Umebarikiwa, kwa kuwa kama alivyofanya Imam Hussein (AS), umewatoa wapendwa wako katika msafara wa Karbala katika njia ya haki.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu akupe uponyaji wa haraka na kamili kutokana na majeraha yaliyosababishwa na shambulio hili la kinyama, na tunakuombea mafanikio yanayozidi kuongezeka pamoja na ulinzi wa Mwenyezi Mungu.
Kwa miaka mingi tumekuwa tukisikiliza hotuba zako zenye kina kikubwa , zilizojaa elimu, utamaduni, ufahamu mpana, maarifa ya kina kuhusu Iran na mataifa mengine, uchambuzi makini wa matukio, upeo wa kuona yajayo, pamoja na utambuzi wa nguvu na udhaifu wa Umma wa Kiislamu na njia za kushinda changamoto. Pamoja na hadhi yako ya juu katika ijtihad na ubora wa darsa zako za kielimu za ngazi ya juu, daima tuliamini kuwa Mwenyezi Mungu amekuandalia daraja kubwa.
Na pale Mwenyezi Mungu alipokuokoa bila madhara makubwa kutoka chini ya vifusi vya shambulio la mabomu lililofanywa na utawala wa kihalifu wa Kizayuni wa Marekani, imani yetu katika ukweli wa matarajio hayo ilizidi kuimarika.
Ewe mrithi bora wa watangulizi bora! Umesimama si tu kutibu majeraha yako mwenyewe, bali pia kuponya nyoyo zetu na kuuongoza Umma wa Kiislamu kutoka ushindi mmoja kwenda mwingine , hadi siku bendera itakapokabidhiwa kwa Imam al‑Mahdi (roho zetu ziwe fidia kwake).
Hivyo basi, tukimtegemea Mwenyezi Mungu, fahamu kwamba mhimili mzima wa Muqawama, wapiganaji wake na makamanda wake, utatii amri zako kama walivyokuwa kwa amri za baba yako aliyeuawa shahidi. Mwenyezi Mungu akujaalie uendelee kuwa chini ya ulinzi Wake daima.
4339733