IQNA

Barua ya Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa Iran kwa Waislamu na Serikali za Kiislamu.

12:28 - March 17, 2026
Habari ID: 3482064
IQNA-Katika taarifa yenye vipengele sita iliyoelekezwa kwa serikali za nchi za Kiislamu, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema: “Lazima muamue msimamo wenu katika Vita vya Ramadhani, je, mnasimama upande wa nchi ya Kiislamu ya Iran, au upande wa Marekani na Israel?”

Barua ya Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa Iran kwa Waislamu na Serikali za Kiislamu.

Kwa mujibu wa taarifa, Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, alitoa taarifa hiyo siku ya Jumatatu ambapo amezihutubu serikali za Kiislamu kwa kuandika hivi:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Kwa Waislamu wa dunia na serikali za Kiislamu

1. Iran ilikabiliwa na shambulio la hila la Marekani na utawala wa Kizayuni, tena wakati wa mazungumzo. Shambulio hilo lilikuwa na lengo la kuigawa Iran vipande vipande. Katika shambulio hilo, Kiongozi mkuu na mwenye kujitolea wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na baadhi ya raia wa kawaida na makamanda wa kijeshi waliuawa shahidi; hivyo wavamizi wamekabiliwa mapambano kitaifa na ya Kiislamu ya watu wa Iran.

2. Mnajua kwamba, isipokuwa katika matukio machache sana na hasa katika kauli za kisiasa, hakuna serikali ya Kiislamu iliyokuja kusaidia taifa la Iran. Hata hivyo, watu wa Iran kwa azma na irada thabiti walimdhibiti adui muovu, kiasi kwamba leo adui hajui namna ya kujinasua kutoka katika mkwamo huu wa kimkakati.

3. Iran itaendelea na njia ya muqawama dhidi ya Shetani mkubwa na mdogo (Marekani na Israel). Lakini je, mwenendo wa baadhi ya serikali za Kiislamu unaligana na kauli ya Mtume Muhammad (SAW) aliyesema: “Asiyeitikia kilio cha Muislamu si Muislamu.” Je, huu ni Uislamu wa aina gani?

4. Baadhi ya nchi zimeenda mbali zaidi na kusema kwamba kwa kuwa Iran imelenga kambi za Marekani pamoja na maslahi ya Marekani na Israel katika nchi hizo, basi Iran ni adui yao! Je, Iran inapaswa kukaa kimya wakati mashambulizi dhidi yake yanafanywa kutoka katika kambi za Marekani zilizoko katika nchi zenu? Wanatafuta visingizio; leo katika upande mmoja wa mapambano wapo Marekani na Israel, na upande mwingine ipo Iran ya Kiislamu pamoja na nguvu za muqawama. Ninyi mko upande gani?

5. Fikirieni mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu. Mnajua kwamba Marekani haina uaminifu kwenu, na Israel ni adui yenu. Chukueni hata dakika moja kufikiria juu yenu wenyewe na mustakabali wa eneo hili. Iran inawatakia mema na haina nia ya kuwatawala.

6. Umoja wa Umma wa Kiislamu, kwa nguvu zake zote, unaweza kuhakikisha na kudhamini usalama, maendeleo na uhuru wa nchi zote.

Mja wa Mwenyezi Mungu

Ali Larijani

16/03/2026

 /4341253

captcha