Kauli za hivi karibuni za qari wa Kuwait, Mishary al‑Afasi, za kuhalalisha mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na ukosoaji wake kuhusu Waislamu wanaounga mkono Iran, zimeibua malalamiko kutoka pande mbalimbali.
Hussein Hamdan, mwalimu na qari mkongwe wa Lebanon ambaye amehudumu pia kama jaji katika mashindano mengi ya kimataifa ya Qur’ani, aliambia IQNA katika mahojiano kuwa misimamo ya hivi karibuni ya al‑Afasi hailingani na maadili ya Qur’ani.
Hamdan alielekeza kwenye Aya ya 47 ya Surah Al‑Ma’idah: “... Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wapotofu.”
Akasema pia kuwa Qur’ani inawakemea baadhi ya wanaosoma Qur’ani bila kuyazingatia mafunzo yake, na kuongeza kuwa maneno ya qari huyu hayampendezi Mwenyezi Mungu bali huwafurahisha wale walio madarakani.
Kuhusu athari za kauli za al‑Afasi katika mtazamo wa watu katika ulimwengu wa Kiislamu, Hamdan alisema fikra na mitazamo hiyo inaweza kuathiri wale tu wanaotanguliza maslahi ya kidunia kuliko dini yao.
“Lakini wenye busara humlaumu kwa matendo yake yasiyofaa,” akaongeza.
Alipoulizwa kuhusu wajibu wa wanafunzi wa Qur’ani, wasomaji na wahifadhi katika kukabiliana na mitazamo kama hiyo, Hamdan alisema kuwa jamii ya Kiislamu yenye ufahamu, pamoja na wahudumu wa Qur’ani, wanapaswa kusisitiza kuwa Qur’ani ni kitabu cha tafakuri, si cha kusomwa kwa sauti nzuri pekee au mchezo wa lafudhi.
“Ujumbe wa Qur’ani ni kuiweka haki mahali pake,” alisisitiza.
Kuhusu hoja ya kuondoa tilawa za qari huyo katika vyombo vya habari kama redio, televisheni na mitandao ya kijamii, Hamdan alisema kuwa inafaa tilawa hizo kuondolewa ili jamii isidhani kuwa uzuri wa sauti pekee ndio kiini cha dini.
Alipoulizwa kwa nini mtu mwenye sauti mashuhuri kama al‑Afasi anachukua msimamo kama huo, qari huyo kutoka Lebanon alisema kuwa umahiri wake katika herufi na lahaja ni kama mtu anayejua kuzungumza bali hakujali mipaka ya adabu na maadili.
Kuhusu mwitikio wa wananchi na watendaji wa Qur’ani nchini Lebanon, Hamdan alisema: “Hakika, msimamo huu wa qari huyu utakumbana na kukataliwa na hata kubezwa na wasomaji wa Qur’ani nchini Lebanon na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu.”
Alisisitiza kuwa ili kufaidika na mafundisho halisi ya Qur’ani na kuepuka upotofu, mtu anapaswa kuielewa Qur’ani kwa undani, dhahiri na batini. Akarejea Aya ya 24 ya Surah Muhammad:
“Je, hawatafakari juu ya Qur’ani, au je, mioyo yao imefungwa?”
Pia alikumbusha simulizi ya Balaam Ba‘ura, mja mwema wa Bani Isra’il, ambaye maombi yake yalikuwa yakikubaliwa lakini baadaye akachagua njia isiokuwa ya haki na kuongozwa na upotofu.
3497273