Kitengo cha Elimu ya Qur’ani kwa Wanawake cha Astan kinaendesha programu hiyo kupitia vituo saba vilivyowekwa katika maeneo mbalimbali yanayohudumia mazuwari wanawake.
Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Astan, wafanyakazi na wajitolea wanawake 26 wanashiriki katika utekelezaji wa programu hiyo. Vituo hivyo vinatoa huduma mbalimbali, zikiwemo kusahihisha usomaji wa Surat Al-Fatiha na sura fupi za Qur’ani, kujibu maswali ya Qur’ani, kufuatilia usomaji, pamoja na kusahihisha makosa ya matamshi na ya kanuni za Tajwidi.
Huduma hizo zinachangia kueneza utamaduni wa Qur’ani na kuongeza uelewa wa kidini miongoni mwa waumini wakati wa ziara ya Arbaeen.
Dalal al-Tabatabai, mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Qur’ani kwa Wanawake, alisema programu hiyo ni sehemu ya dhamira ya Astan ya kuitumikia Qur’ani Tukufu na kueneza mafundisho yake.
Alisema vituo hivyo vimeshuhudia ongezeko la idadi ya mazuwar wanawake kutokana na huduma za kielimu na za uongofu vinazotoa. Huduma hizo huwasaidia wanawake kusahihisha usomaji wao na kuimarisha uhusiano wao na Qur’ani Tukufu.
Al-Tabatabai aliongeza kuwa kitengo hicho kinatumia fursa ya mazingira yenye baraka ya ziara ya Arbaeen kuimarisha imani kwa kusambaza nakala za Qur’ani, vitabu vya dua na zawadi zilizobarikiwa, pamoja na kuwahimiza mazuwar wanawake kutumia safari hiyo ya ibada kwa ajili ya kusoma na kuhifadhi Qur’ani Tukufu.
Aliendelea kusema kuwa shughuli za vituo vya Qur’ani zinaendelea kwa ushirikiano na wafanyakazi wa Kitengo cha Elimu ya Qur’ani kwa Wanawake. Shughuli hizo zinaakisi mkabala wa Astan wa kuunganisha uhamasishaji wa Qur’ani na huduma za moja kwa moja kwa mazuwar wakati wa ziara ya Arbaeen.
3498501