Wizara ya Awqaf na Masuala ya Kiislamu ya nchi hiyo, kwa ushirikiano na Wizara ya Mazingira, siku ya Jumapili ilizindua vituo vya kutoa mafunzo bila malipo katika majira ya kiangazi kwa ajili ya kuhifadhi Qur’ani kwa wavulana na wasichana.
Mpango huo wa miezi miwili unafanyika chini ya kaulimbiu: “Mazingira Safi na Jamii Iliyo Bora Zaidi.” Katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Bustani za Mfalme Hussein, Waziri wa Awqaf na Masuala ya Kiislamu, Mohammad Khalaileh, alisema vituo vya mwaka huu vinawakilisha mradi mpana wa kielimu na kitaifa unaolenga kukuza maadili ya Kiislamu ili yawe mwenendo wa vitendo katika jamii.
Khalaileh alibainisha kuwa wizara imeanzisha vituo hivyo mwaka huu kwa ushirikiano na Wizara ya Mazingira ili kuimarisha utamaduni wa kulinda mazingira kama sehemu muhimu ya mafundisho ya Uislamu.
“Qur’ani Tukufu haijikiti tu katika kuhifadhi na kusoma, bali pia inalingania kujenga watu wema wanaoitunza na kuilinda ardhi,” alieleza.
Aliongeza kuwa shughuli za mpango huo zinalenga kudumisha usafi wa mazingira na kuhifadhi miundombinu ya umma, akisisitiza kuwa usafi ni “thamani ya kidini, kitamaduni na kiafya inayodhihirisha ustaarabu wa jamii.”
Kwa mujibu wake, wizara inapanga kufungua takribani vituo 3,000 vya majira ya kiangazi kote nchini mwaka huu, huku ikitarajia zaidi ya wanafunzi 200,000 wa kike na wa kiume kufaidika na huduma hizo.
Alifafanua kuwa ushiriki katika vituo hivyo hauna malipo hata kidogo na kwamba masomo yatafanyika misikitini chini ya usimamizi wa walimu wa kiume na wa kike walioteuliwa wenye sifa stahiki.
Kuhusu shughuli nyingine, alisema mpango huo pia unajumuisha mashindano ya kitamaduni na kidini, matukio ya michezo pamoja na kampeni za kujitolea kusafisha maeneo ya misikiti na vituo vya majira ya kiangazi.
Alitangaza kuwa madarasa kwa wavulana yatafanyika siku za Jumapili, Jumanne na Alhamisi, huku masomo kwa wasichana yakifanyika siku za Jumamosi, Jumatatu na Jumatano.
Aidha alibainisha kuwa masomo yatafanyika katika viwanja vya misikiti na vituo vya Qur’ani, akiongeza kuwa wizara imetangaza maeneo yaliyoidhinishwa kote nchini pamoja na majina ya wasimamizi wa kiume na wa kike kupitia tovuti yake na kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
3498010