IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu, Mjumuiko wa Viongozi wa Baadaye

19:05 - October 04, 2016
Habari ID: 3470598
Mwambata wa Utamaduni wa Iran nchini Tanzania amesema Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanachuo Waislamu ni mjumuiko wa viongozi wa baadaye wa ulimwengu wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Ali Baqeri amesema mashindano hayo ni harakati ya Qura'ni yenye kudumu na ambayo inaweza kuwa na mchango mkubwa wa kuleta umoja wa Kiislamu katika mhimili wa Kitabu cha Allah.

Akademia ya Elimu, Utamaduni na Utafiti Iran (ACECR) imekuwa ikiandaa mashindano hayo ya Qur’ani ya wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu tokea mwaka 2006 kwa lengo la kuimarisha umoja wa Kiislamu na kuleta ushirikiano miongoni mwa wanafunzi Waislamu sambamba na kuinua kiwango cha harakati za Qur'ani.

Mji mtakatifu wa Mashhad utakuwa mwenyeji wa mashindano yajayo ya kimataifa ya Qur'ani ya wanachuo Waislamu hayo na inatazamiwa kuwa mashindano hayo yatafana sana kwa kuzingatia hadhi ya mji huo. Mashindano hayo yanatazamiwa kufanyika Januari 1-4 mwaka 2017 katika mji huo ulio kaskazini mashariki mwa Iran.

Baqeri amesema mashindano hayo ambayo hufanyika katika kategoria za qiraa (kusoma) na hifdhi (kuhifadhi) Qur'ani Tukufu ni hatua ya kustawisha utamaduni wa Qur'ani miongoni mwa wanafunzo Waislamu katika vyuo vikuu kote duniani. Amesisitiza kuwa mashindano hayo huimarisha umoja na kusaidia kuzima njama za maadui za kuibua mifarakano baina ya Waislamu.

Aidha amesema mashindano hayo huwaleta pamoja Waislamu kutoka madhehebu mbali mbali kwani wote wanajitambua kama Waislamu ambao wanaamini kitabu kimoja.

Akademia ya Elimu, Utamaduni na Utafiti Iran (ACECR) imekuwa ikiandaa mashindano ya Qur’ani ya wanachuo Waislamu baada ya kila miaka miwili tokea mwaka 2006 kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano baina ya wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu kote duniani sambamba na kustawisha kiwango cha harakati za Qur’ani katika vyuo vikuu.

3535348

captcha