IQNA

Rais wa Indonesia alaani matamshi ya Macron kuhusu Uislamu, ataoa wito wa umoja

12:01 - November 01, 2020
Habari ID: 3473316
TEHRAN (IQNA)- Rais Joko Widodo wa Indonesia amelaani kauli ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa dhidi ya Uislamu na kusema mtawala huyo amewatusi Waislamu wote duniani.

Akizungumza Jumamosi, amesema kauli ya Macron inaweza kuibua migongan baina ya wafuasi wa dini mbali mbali duniani katika kipindi hiki ambacho dunia inahitaji umoja ili kukabiliana na janga la COVID-19.

“Uhuru wa maoni haupaswi kutumiwa kwa njia ambayo inavunjia heshima matukufu ya kidini,” aliongeza rais wa Indonesia katika mkutano na waandishi habari kwa njia ya intaneti.

Aidha alilaani vikali hujuma za kigaidi ambazo zilijiri Paris na Niece Ufaransa na kusema Indonesia inatoa wito wa umoja na kustahamiliana kidini kwa ajili ya kujenga dunia bora.

Rais wa Indonesia amebainisha masikitiko yake kuwa Macron amenasibisha hujuma za kigaidi na Uislamu na kusema hilo ni kosa kubwa. “Ugaidi ni ugaidi. Magaidi ni magaidi. Ugaidi hauna uhusiano wowote na dini yoyote ile,” ameongeza.

Rais Macron wa Ufaransa anaendelea kukosolewa na Waislamu kimataifa kutokana na matamshi yake ya kuutusi Uislamu na Mtume Muhammad SAW. Matamshi hayo yameibua maandamano ya kumlaani huku kukianzishwa kampeni ya kutaka bidhaa zote za Ufaransa zisusiwe.

3472991

captcha