IQNA

Wanandoa wazee wa Kiindonesia, wenye umria wa miaka 100, 95 wanaelekea Hija

20:33 - May 17, 2025
Habari ID: 3480697
IQNA – Mwanamume mwenye umri wa miaka 100 na mke wake wa miaka 95 kutoka Aceh ya Kati nchini Indonesia wanajiandaa kujiunga na mamilioni ya Waislamu katika ibada ya Hija ya mwaka huu, wakionyesha imani thabiti na uthabiti wa mwili katika uzee wao.

Muhammad Dahlan na mkewe, Dahniar, wakazi wa Tapak Moge Timur katika eneo la Kute Panang, wanatarajiwa kuondoka Mei 20 kama sehemu ya kundi la tatu la Waislamu kutoka Aceh wanaoelekea Hija kupitia kituo cha kuondokea cha Jakarta, kwa mujibu wa ripoti ya Jakarta Globe.

Licha ya umri wake mkubwa, Dahlan bado ana afya njema na ni mchangamfu, akiendelea kulima shamba lake la kahawa. Ameshapitia uchunguzi wa kimatibabu na amethibitisha kuwa hali yake ni nzuri, akisema wiki hii nyumbani kwake, “Daktari alisema hakuna tatizo. Niko salama.”

Mkewe, Dahniar, naye alielezea matumaini sawa, akisema kuwa wamejizatiti kikamilifu, kimwili na kiroho, kwa ajili ya safari hii tukufu.

Hii ni safari yao ya tatu kwenda Makka, baada ya hapo awali kutekeleza Umrah mara mbili. Baada ya Umrah ya pili, walijiandikisha kwa Hija ya faradhi mnamo 2019, bila kutarajia kuwa nafasi yao ingefika haraka.

Kujumuishwa kwao katika Hija ya mwaka huu ni sehemu ya mgawo maalum wa nafasi 219 zilizotengwa kwa mahujaji wazee kutoka Aceh, kulingana na Azhari, mkuu wa ofisi ya wizara ya masuala ya kidini ya Indonesia katika mkoa huo.

Nafasi hizi zinapewa kipaumbele kwa wazee waliokuwa kwenye foleni kwa angalau miaka mitano, wakichaguliwa kulingana na umri. Azhari alifafanua kuwa bila mpango huu, Dahlan angalilazimika kusubiri hadi mwaka 2044 kupata fursa yake.

Kwa kuhakikisha faraja na urahisi, mahujaji wazee wamepangiwa malazi katika ghorofa ya chini ya hosteli ya Hija na wanapata huduma maalum katika safari yao yote.

Azhari alisisitiza kuwa safari ya wanandoa hao ni ishara kuwa umri haupaswi kuwa kizuizi cha kutimiza matamanio ya kiroho.

3493109

Kishikizo: indonesia hija
captcha