IQNA

Quds Tukufu hatarini

Jordan yaonya kuhusu mipango ya Israel ya kuyahudisha maeneo ya Kiislamu, Kikristo mjini Al-Quds

13:50 - September 07, 2024
Habari ID: 3479392
IQNA - Wizara ya Wakfu ya Jordan imetahadharisha kuhusu kushadidi hatua za utawala wa Kizayuni zenye lengo la kueneza Uyahudi katika maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo katika mji mtakatifu wa al-Quds (Jerusalem).

Wizara hiyo ilitoa wito kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kutimiza wajibu wao kuhusu mji huo mtakatifu.

Imesema mataifa ya Kiarabu na Kiislamu yanapaswa kutoa shinikizo kwa utawala wa Israel na kuzuia majaribio yake ya kutaka kuudhibiti  Msikiti wa Al-Aqsa ulioko mjini al Quds, tovuti ya al-Mashhad al-Arabi iliripoti.

Wizara hiyo iliitaja hali ya sasa ya al-Quds kuwa ni hatua hatari katika majaribio ya kubadilisha hadhi ya kihistoria na kisheria ya maeneo ya Kiislamu na Kikristo ya mji huo.

Kabla ya hapo, Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Jordan, Mohammad Khalaileh alikashifu kukithiri na ukiukwaji wa hadhi ya Msikiti wa Al-Aqsa unaofanywa na maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na walowezi wa Kizayuni wenye itikadi kali wanaopata himaya ya Israel.

Alionya juu ya madhara mabaya ya uvamizi huo na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa kwa waumini wa Kiislamu wanaofika katika Msikiti wa Al-Aqsa.

Khalaileh alisisitiza kwamba Waislamu wana haki za kidini, kihistoria na kisheria kwa Msikiti wa Al-Aqsa, akiongeza kuwa msikiti huo ni eneo la Kiislamu pekee, na majaribio yoyote ya kugawanya au kudhibiti eneo hilo takatifu hayakubaliki.

 4235133

captcha