IQNA

Tunisia yasisitiza kutoanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel

18:07 - December 23, 2020
Habari ID: 3473484
TEHRAN (IQNA) - Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Tunisia imeashiria juhudi za baadhi ya mataifa ya kieneo za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kusisitiza kwamba, serikali ya Tunis haina mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu.

Taarifa rasmi ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Tunisia imesisitiza kuwa, tetesi na uvumi unaoenea kwamba, nchi hiyo ina mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel hauna ukweli wowote na kwamba, misimamo ya Tunis haiwezi kuathiriwa na mabadiliko ya kimataifa.

Aidha sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kwamba, madai kwamba, Tunisia inataka kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel yanapingana na misimamo rasmi ya nchi hiyo ya kutetea malengo ya Palestina pamoja na haki za wananchi hao madhulumu.

Msimamo huo unatangazwa siku chache tu baada ya Waziri Mkuu wa Tunisia Hichem Mechichi kusisitiza kuwa nchi yake haina ajenda ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hivi karibuni, Morocco ilikuwa nchi ya nne ya Kiarabu kuanzisha uhusiano na Israel tokea mwezi Agosti wakati mtawala wa Marekani anayeondoka, Donald Trump alipoanzisha mkakati wa kuzishinikiza nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala huo bandia.

Mbali na Morocco, nchi zingine za Kiarabu ambazo zimeanzisha uhusiano na Israel hivi karibuni ni pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan ambazo zimeanzisha uhusiano na utawala huo dhalimu katika fremu ya njama za Marekani-Kizayuni za kudhoofisha uungaji mkono wa nchi za Kiarabu kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina. 

3942869

Kishikizo: tunisia palestina israel
captcha