IQNA

Hizbullah yatahadharisha kuwa itatoa jibu kali kwa hujuma yoyote ya Israel

11:35 - February 17, 2021
Habari ID: 3473657
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel na kuutaka kutocheza na moto huku akisisitiza kuwa hujuma yoyote ile ya Israel dhidi ya Lebanon itakabiliwa na jibu kali kutoka Hizbullah.

Sayyid Hassan Nasrallah ameyasema hayo katika hotuba ya Televisheni Jumanne usiku kwa mnasaba wa kukumbuka kuuawa shahidi makamanda wa ngazi za juu wa Hizbullah akiwemo Shahidi Imad Mughniyeh ambaye aliuawa Syria mnamo Februari 2008.

Sayyid Nasrallah amesema Hizbullah haitaki makabiliano ya kijeshi lakini itapambana kwa nguvu zaidi ya miaka ya nyuma iwapo italazimishwa kuingia vitani.  Katibu Mkuuu wa Hizbullah amesema utawala haramu wa Israel katu haijawahi kufungamana na sheria za kimataifa na huharibu miji na kuua raia katika vita vyake vyote.

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu wa Hizbullah amepongeza 'hatua chanya' iliyochukuliwa na Marekani ya kuacha kuunga mkono hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen. Sayyid Nasrallah amesema uamuzi huo umetokana na kusimama kidete Wayemeni.

Katika sehem nyingine ya hotuba yake Kiongozi wa Hizbullah amesema leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dola lenye nguvu na uwezo mkubwa katika eneo la Asia Magharibi. Amesema Iran imeweza kusimama kidete mbele ya mashinikizo na vikwazo vya Marekani na waitifaki wake.

Kuhusiana na mwamako wa wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa, Sayyid Nasrallah amesema Wabahrain wakiongozwa na Sheikh Issa Qassim wamejitolea muhanga kwa ajili ya uhuru.

Katibu Mkuu wa Hizbullah pia amekosoa mapatano ya nchi chache za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema utawala wa Kizayuni umekuza kupita kiasi mapatano hayo kwa maslahi ya kisiasa.

"Waarabu ambao wanajigama kuhusu safari zao Israel hawahakilishi Waislamu zaidi ya bilioni 1.5 duniani," amesema Sayyid Nasrallah.

3474005

captcha