Abdul-Malik al-Houthi ameyasema hayo katika hafla ya jana Jumapili ya kuadhimisha Maulidi na kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) mjini Sana’a ambapo maelfu ya Wayemeni walikuwa wamekusanyika.
Amesema shambulio la hivi karibuni la makombora la Yemen dhidi ya mji wa Tel Aviv huko Israel ni sehemu ya awamu ya tano ya operesheni za kukabiliana na Israel.
Al Houthi amesisitiza kuwa, operesheni dhidi ya Israel zitaendelea hadi utawala huo utakapokomesha mauaji yake ya kimbari huko Gaza na mzingiro wake katika eneo hilo.
"Operesheni zetu zitaendelea maadamu uchokozi na mzingiro wa Wazayuni dhidi ya Gaza vinaendelea. Msimamo wetu unaendelea kuwa thabiti hadi pale Palestina itakapokombolewa kutoka kwenye makucha ya wavamizi,” amesema kiongozi wa Ansarullah.
Mapema jana Jumapili, jeshi la Yemen lilishambulia eneo la jeshi la Israel huko Tel Aviv kwa kombora jipya la balistiki la Hypersonic.
Jeshi la Israel limethibitisha kutokea shambulizi hilo na kukiri kuwa mifumo yake ya ulinzi umeshindwa kuzuia kombora hilo.
Abdul-Malik al-Houthi amesisitiza kuwa: “Waislamu lazima waendelee kuwa imara na wastahimilivu katika kukabiliana na matatizo na changamoto. Waanapaswa kuwa wanyoofu, wenye bidii na wepesi katika kutekeleza majukumu yao.”
Msemaji wa jeshi la Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree amesisitiza kuwa kombora hilo jipya la balistiki la Hypersonic lilirushwa hadi Tel Aviv kwa kutumia muda wa dakika 11 na sekunde 30 katika umbali wa kilomita 2040; jambo lililowatia kiwewe na hofu Wazayuni na kupelekea Wazayuni zaidi ya milioni mbili kukimbilia mafichoni.
3489911