"Adui Muisraeli anafuata mpango unaoitwa Ukanda wa David, ambao unalenga kunyakua ardhi zaidi na kupanua maeneo yanayokaliwa na Marekani na yanayoshikiliwa na Wakurdi kwenye ukingo wa Mto Euphrates," Abul-Malik al-Houthi alisema katika hotuba ya televisheni Alhamisi.
Amegusia ndoto ya Israel ya kufika mto Euphrates na kusema utawala huo unaiona hali iliyojitokeza kuwa ni muafaka kwa vile hakuna kikwazo chochote katika uvamizi wake nchini Syria.
Jeshi la Israel, alisema, linaharibu vituo vya kijeshi vya Syria ambavyo ni vya taifa la Kiarabu na ni muhimu kukabiliana na vitendo vya uchokozi vya utawala wa Tel Aviv.
Kiongozi huyo wa Ansarullah aliwakashifu watawala wapya wa Syria kwa kutofanya lolote kulinda silaha za kistratijia na maeneo ya kijeshi nchini humo na hivyo kuwaacha Wasyria katika hatari ya kushambuliwa na Israel.
"Hatua ya adui Muisraeli kuharibu uwezo wa kiulinzi wa Syria unawakilisha uchokozi wa jinai, ukiukaji wa wazi, na shambulio dhidi ya mamlaka yake ya kitaifa," alisema.
Aidha ameonya kuwa Israel inafuatilia mpango wa kumiliki ardhi yenye rutuba kusini mwa Syria.
Al Houthi kisha ameikashifu Marekani na washirika wake wa Magharibi kwa kutaja uchokozi wa Israel dhidi ya Syria kama "vitendo vya kujilinda," na kusema kwamba ukatili huo ni ukiukaji wa wazi wa kanuni zote za kimataifa.
Aliashiria undumakuwili wa Magharibi, amesema kujilinda kwa makundi ya Muqawama huko Gaza na Lebanon kunasawiriwa kama ugaidi.
Al Houthi amesema machafuko nchini Syria yamewezesha unyakuzi zaidi wa ardhi wa Israeli huku kukiwa na ukimya wa makundi yenye silaha na kutochukua hatua.
Zaidi ya hayo, amesema kadhia ya Palestina ni suala kuu la ulimwengu wa Kiislamu, na Israel ni tishio kubwa kwa watu wote hususan Waarabu.
Amesisitiza kuwa watawala hao wapya wa Syria wameamrishwa kutotoa maoni yoyote dhidi ya Israel, na kusema kuwa Waislamu wanapaswa kuilinda Gaza kama vile Wazungu wanavyoiunga mkono Ukraine.
Amesema kutochukua hatua kwa nchi za Kiislamu kumeipa Israel ujasiri wa kuendelea na ajenda yake ya kukalia kwa mabavu.
Al Houthi amesisitiza kuwa wanajeshi wa Yemen wataendelea na operesheni zao dhidi ya Israel ili kuwaunga mkono Wapalestina na makundi yao ya muqawama.
Amesema katika kipindi cha wiki moja pekee, makombora ya Yemen yameshambulia maeneo kadhaa ya Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kusababisha uharibifu mkubwa.
3491122